Na Amina Hezron
Morogoro
Kwa kutambua uhitaji mkubwa wa damu hasa kwa Mkoa wa Morogoro,
Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA) na Chuo cha
Afya Hermargs ambao ni wanachama wa klabu inayojihusisha na masuala ya
uchangiaji wa damu ROTARACT, wameungana
kuchangia damu ili iweze kusaidia kupunguza uhitaji mkubwa wa damu na kusaidia
jamii na watu wenye uhitaji.
Mlezi wa kikundi cha Rotaract SUA Prof. Robinson Mdegela akizungumza na vijana
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mlezi wa kikundi cha Rotaract SUA Prof. Robinson Mdegela, amesema Mkoa wa Morogoro ni moja ya Mikoa ambayo imekuwa ikipokea majeruhi wengi pale zinapotokea ajali hivyo kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
“Wamefanya kazi nzuri ambayo ni mbegu ya kuzidi
kuhamasishana na kusaidiana ili changamoto ya ukosefu wa damu isiendelee kuwepo
na vijana wetu hawa wanawajibu wa kufanya changizo kama walivyofanya siku ya
leo ili iwe chachu kwa jamii na vijana wengine lakini pia kutoa mchango wao kwa
jamii “, alisema Profesa Mdegela.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Afya Hermargs, ambaye ni mwenyeji wa zoezi hilo, Benedict Lubusha,
amewashukuru walezi wa vikundi vyote ambavyo vimewazesha kufanyika kwa zoezi
zima la uchangiaji wa damu salama, itakayosaidia kuokoa maisha ya makundi
maalum.
Naye, mmoja wa wanafunzi waliojitokeza kuchangia damu kutoka SUA, Khatibu Mgunya, amewataka vijana kuwa na moyo wa kujitolea kwa kujijengea mazoea ya kwenda kuchangia damu mara kwa mara, ili kuepusha vifo vya watoto na wajawazito vinavyotokana na kukosekana kwa damu.
Kwa upande wake Muuguzi na Mratibu wa
Kitengo cha Damu Salama kutoka kitengo cha Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, Vaileth Mrija amewataka wananchi kuhamasika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watoto ambao wana matatizo ya
seli mundu pamoja na magonjwa ya Kansa ambao nao wamekuwa na uhitaji mkubwa wa
damu.
0 Comments