Na Amina Hezron
Njombe
Serikali kupitia Mamlaka zake za
uhamasishaji, uratibu, usimamizi, uendelezaji na udhibiti wa dawa asili nchini
imeshauriwa kuhakikisha watengenezaji wa dawa hizo hawachanganyi dawa za asili
na zile za kisasa ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa watumiaji.
Ushauri huo umetolewa na Kiongozi
wa Mradi wa Utafiti unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wa Kuongeza
Ubunifu katika Mimea dawa ili kuboresha Maisha (GRILI) Dkt. Faith Mabiki wakati
wa mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa mradi huo unaoendelea mkoani Njombe.
Kiongozi wa Mradi wa Utafiti Dkt. Faith Mabiki akitoa wasilisho lake
Dkt. Mabiki amesema lengo la kufanya
tafiti hizo pamoja na Serikali ni kuhakikisha dawa za asili nchini zinakuwa
bora na kufikia viwango vya kimataifa na kuweza kusafirishwa nje ya nchi
Kwa upande wake Dkt. Doreen Ndosi
kutoka SUA amesema katika wakati huu ambao dunia inakabiliana na changamoto ya
usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kisasa, ni lazima suala ya udanganyifu wa
baadhi ya waganga wa tiba asili uliobainika wa kuchakachua dawa za asili na za
kisasa utafutiwe ufumbuzi maana unachangia katika tatizo hilo.
Naye Kiongozi wa upimaji wa dawa
asili dhidi ya virusi katika Mradi wa GRILI ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la kuendeleza Viwanda Tanzania (TIRDO), Prof. Madundo Mtambo
amependekeza tafiti zaidi zifanyike ili kuisaidia Serikali kupata Ushahidi wa
kutosha na kufanya maamuzi sahihi katika suala hili linalogusa afya za binadamu
na Wanyama.
0 Comments