Na Amina Hezron
Mbarali
Kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji na uoto wa asili
uliofanyika kando kando ya Mto Mbarali
wa mkoani Mbeya, uliotokana na shughuli za kilimo na ufugaji, mradi wa Eflows
unatarajia kuanzisha vitaru vya miti rafiki zaidi ya laki moja kwa ajili ya
kupanda kandokando ya mto huo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kiongozi wa mradi huo Prof.
Japhet Kashaigili, kufanya ziara kandokando ya mto huo akiwa ameambatana na
kiongozi wa bonde la mto Rufiji, Jumuiya za watumia maji na Viongozi wa skimu
ya umwagiliaji ya Igomelo kwa lengo la kwenda kufanya tathimini katika eneo
hilo
Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni kiongozi wa mradi huo akizungumza na wadau hawako pichani wilayani Mbarali
“Mradi pamoja na kufanya utafiti lakini pia
tunataka kuwa sehemu ya kutatua baadhi ya changamoto na kutokana na hali ilivyo
mbaya kwenye vyanzo vya maji vya mto huu na kandonkando ya mto hatua ya kwanza
tunaanzisha vitalu vya miti ili ipandwe kwenye maeneo yote baada ya kupata
ushauri wa aina ya miti inayofaa kutoka kwa wenzetu wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania TFS Wilayani Mbarali” Alisema Prof. Kashaigili.
Amesema hawawezi kusubiri hadi mwisho wa utafiti wao ndio
wafanye kazi ya kurekebisha makosa ambayo yanaonekana waziwazi hivyo lazima
wapande miti rafiki ili kurudisha uoto wa asili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Skimu ya umwagiliaji ya Igomelo
Bi. Aurelia Kayombo, amemshukuru Mkuu wa Mradi huo kwa kufanya ziara hiyo kwa
pamoja na kuwapatia elimu kuhusu sheria za mazingira na uhifadhi wa mito.
“Ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa na
nikiri kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanyika hatukuwa tunafahamu lakini kupitia
ziara hii tumeweza kuona na sasa tunakwenda kuitisha kikao na wananchama wetu
wote na kufanya ziara kama hii na ikiwezekana na viongozi wa wilaya nao wawepo
ili tuweke makubaliano ambayo yatasaidia kulinda mto huu muhimu” Alieleza
Kayombo
Eneo la Mto Mbarali likitiririka maji
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Mto Mbarali
(JUWAMBA) Bw. Siasa Shabani, amesema wamefanya kazi kubwa katika kutoa elimu na
kuwakamata watu ambao wamekuwa wakivunja sheria na taratibu walizojiwekea ili
kupunguza idadi ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji lakini tatizo bado
linaendelea.
0 Comments