Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 29 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake imeunda kikosi kazi maalum cha wataalam wabobezi kinachoendelea kufanya mapitio na kuainisha mapungufu yote ambayo yamejitokeza kwenye Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa watumishi (OPRAS) ili kupendekeza mfumo mpya wa kielektroniki wa wazi na rafiki ambao utaondoa upendeleo, udanganyifu na kuongeza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
“Katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais, Ofisi yangu imeamua kuchua hatua haraka iwezekanavyo kuunda timu hii maalum ya wataalam wabobezi ili kuhakikisha tunapata mfumo bora, imara na wenye tija ambao utaondoa changamoto za utekelezaji zilizojitokeza katika mfumo wa OPRAS unaotumika hivi sasa, uliosanifiwa mwaka 2004,” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, timu hiyo ya wataalam imemthibitishia kuwa, mfumo huo mpya wa kielektroniki wa upimaji wa utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja unaopendekezwa utakuwa ni mfumo rafiki na wenye manufaa kwa Watumishi wa Umma, ambao utarahisisha uandaaji wa mikataba ya utendaji kazi na kutoa fursa ya kujiwekea malengo na shabaha kwa kila mtumishi.
“Mfumo huo mpya utapunguza muda wa Watumishi wa Umma kucheza na makaratasi na utawataka viongozi wenye dhamana ya usimamizi wa watumishi kutimiza wajibu wao kwa kufanya ufuatiliaji, kupima na kutoa mrejesho wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma bila kuwaonea, kuwakandamiza ama kutumia hila ya aina yoyote,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga kuhakikisha mfumo huo mpya wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma uanze kutumika rasmi tarehe 01 Julai, 2022.
Chanzo
|
0 Comments