- Rashid Abdallah
- Mchambuzi Tanzania
Zaidi ya miezi 11 imekatika tangu kifo cha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Seif Sharif Hamad, Februari 17, 2021. Alikuwa mwenyekiti wa pili akitanguliwa na Anna Mghwira, aliyevuliwa uenyekiti baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro 2017.
Mkutano Mkuu maalum wa ACT Wazalendo, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, umemchagua kwa kura nyingi Juma Duni Haji (Babu Duni), kuwa mwenyekiti wake mpya. Atakuwa mwenyekiti wa tatu wa chama.
Lakabu ya Babu Duni imesadifu ukubwa wa umri na ukongwe katika siasa za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika mchuano huo wa ndani ya chama, Babu Duni alimbwaga Hamad Masoud Hamad.
Swali ni: Je, changamoto gani zinazomkabili Mwenyekiti huyo?
Ataendeshaje siasa zake?
Katika wakati huu wa 'katazo' la mikutano ya hadhara, mwenyekiti mpya anakumbwa na changamoto kubwa kama wanayopitia viongozi wengine wa upinzani. Ataendeshaje siasa zake nje ya ofisi wakati kuna marufuku ya kukusanyika?
Upinzani ndani ya Zanzibar una uhuru wa kufanya siasa, ziwe za hadhara au ndani. ACT Wazalendo bado ni chama kichanga, chenye kuhitaji kukua hasa Tanzania Bara. Ili kupata Wabunge wengi zaidi katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025, kutahitajika siasa za majukwaani kutafuta wafuasi wapya.
Chama hicho kilichosajiliwa mwaka 2014, kisingepata nguvu ya haraka kuzitawala siasa za Zanzibar kama si mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) uliosababisha wafuasi wake kuhamia ACT. Uchaguzi wa Oktoba 2020, ACT Wazalendo kikawa ndio chama kikuu cha upinzani Zanzibar.
Ulipoisha uchaguzi wa 2015, ACT Wazalendo ilikuwa na Mbunge mmoja tu, Zitto Kabwe, wa jimbo la Kigoma mjini. Katika uchaguzi uliozongwa na mambo mengi yaliyobishaniwa wa Oktoba 2020, chama hicho kilifanikiwa kupata Wabunge wapya wanne kutokea Zanzibar, ingawa hakikupata mbunge yeyote Tanzania Bara.
Mivutano ya upinzani
Kuna mvutano unaozidi kufukuta kila uchao, kati ya ACT Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kwa hakika vita hivi ni kama vya panzi, chama kinachonufaika ni kile kinachotawala.
Kuwepo kwa ushirikiano wa vyama vya upinzani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananachi (UKAWA), katika uchaguzi wa 2015, kulichangia kwa kiwango kikubwa Chadema upande wa Tanzania Bara kukitia tumbo joto Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu.
Ushirikiano huo pia ulikuwa chachu ya kupatikana kwa mavuno makubwa ya wabunge wa upinzani katika Bunge la baada ya uchaguzi. Mvutano wa sasa wa Chadema na ACT, hauwezi kuwa wa afya panapohusika mapambano dhidi ya chama kinachoshika dola, yaani CCM.
Mvutano wa sasa unachochewa zaidi na kule kutofautiana mbinu za vyama hivyo kuondosha ukandamizaji wa utawala dhidi ya siasa za upinzani; mwenyekiti mpya atakuwa na wajibu wa kutafuta njia ya kuondoa mvutano huu kwa manufaa ya upinzani, kabla ya uchaguzi wa 2025.
Fupa lililomshinda Maalim
Swali la kwanini Maalim Seif hakufanikiwa kuwa Rais wa Zanzibar! Yamkini kutakuwa na majawabu mengi, lakini lile jawabu lililonyooka ni kwamba - chaguzi za visiwa hivyo hufunikwa na matukio mengi yanayotia walakini matokeo yenyewe japo wanaoshinda mara zote husema hushinda kihalali.
Sehemu ya ripoti ya Shirika la Human Rights Watch, iliyochapishwa Novemba 30, 2021 kuhusu yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 visiwani Zanzibar, inaeleza:
"Jioni ya tarehe 26, 27 na 28 mwezi Oktoba vikosi vya ulinzi viliwafyatulia risasi makundi ya watu karibu na vituo vya kupigia kura kisiwani Pemba. Takriban watu tisa waliuawa, akiwemo mwanafunzi wa umri wa miaka 16 na mwanamke mja mzito."
Ripoti hiyo inaendelea, "Oktoba tarehe 28, vurugu ziliongezeka huku Tume ya uchaguzi visiwani Zanzibar ikifanya hesabu ya kura. Wanamgambo wajulikanao kama 'Mazombi' waliwafukuza na kuwapiga watu wakiwemo wale waliokuwa wamefika kwenye kituo cha kuhesabu kura kushuhudia utaratibu wa kuhesabu."
Alipozungumza na BBC juu ya ripoti hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa wakati huo, George Simbachawene alisema: "siwezi kuzungumzia ripoti inayoeleza masuala ya jumla jumla".
Tukirudi nyuma katika uchaguzi wa 2015: "Mabalozi na wawakilishi wa nchi kadhaa za Ulaya na Marekani walitoa tamko la kusikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, bila kuwepo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa." Uchaguzi wa marejeo ambao hata hivyo ulisusiwa na chama kikuu cha upinzani wakati huo, CUF ulifanyika Machi 20, 2016.
Ingawa Tume ya Uchaguzi Zanzibar mara zote hutoa maelezo yanayoashiria chaguzi za visiwa hivyo hufanyika kwa uwazi, uhuru na sawa, upande mwingine wa hadithi kunakuwa na ripoti za waangalizi ambazo huonesha mambo hayakwenda sawa kama yanavyosemwa na ZEC.
Maalim Seif aliondoka duniani bila kufikia lengo lake la kuwa Rais wa visiwa hivyo. Alishiriki mara sita kama mgombea wa Urais. Mazingira ya chaguzi kwa asilimia kadhaa yalichangia lengo hilo kutotimia.
Yule anayevaa viatu vyake sasa, atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kunapatikana mageuzi makubwa katika taasisi muhimu zinazosimamia chaguzi; hasa tume ya chaguzi na vikosi vya usalama ili chaguzi zijazo ziende sawa bin sawiya.
SUK ndio utulivu wa Zanzibar
Januari 12, 2022 Zanzibar ilikuwa na kumbukumbu ya miaka 58 ya Mapinduzi ya 1964. Kwa hakika mapinduzi hayo hayakuleta tu mabadiliko ya kisiasa, pia yalileta msiba mkubwa, pale roho nyingi za wasio na hatia zilipoondoka.
Mwandishi wa kitabu cha "Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar," ndugu Hashil Seif Hashil anaamini mapinduzi hayo yangeepukika kama Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyopendekezwa ingeundwa baada ya Zanzibar kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.
Kwa kuzingatia mivutano ya muda mrefu yanayochochewa kwa sehemu kubwa na siasa za visiwa hivyo. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ina umuhimu wa kipekee kutuliza hali ya mambo. Ilikuwa ni muhimu iwepo baada ya uhuru na inabaki kuwa muhimu hata sasa.
Maalim Seif alishiriki kuasisi muundo huo wa kiutawala. Ni moja ya jambo muhimu ambalo mvaaji wa viatu vyake atakuwa na wajibu wa kuhakikisha SUK inaendelea kuwepo sasa na hata baadaye kwa faida ya utulivu wa visiwa hivyo.
Babu Duni ni mwanasiasa mkongwe mwenye uzoefu wa muda mrefu. Kuvivaa viatu vya Maalim Seif ni kazi moja - kuleta matokeo chanya baada ya kurithi nafasi hiyo ni kazi nyingine. Fursa mbele yake ni kubwa japo hali ya kisiasa Zanzibar na hata kwa Tanzania Bara haijabadilika sana. Hata hivyo, kuna mwangaza wa matumaini kulinganisha na hali iliyokuwepo kati ya 2015 na 2020. Bado kunahitajika muda wa kusubiri kuona anaiandika vipi historia yake.
0 Comments