Na Amina Hezron
Njombe
Wananchi wametakiwa kutotumia dawa za asili bila
kupata ushauri wa wataalamu ili kutumia kwa Kiwango kilichotafitiwa cha mimea
tiba wanayoitumia kwa ajili ya kutibu afya zao kwakuwa kiwango kingi ama
kidogo, vyote vinaweza kuleta madhara mengine katika mwili.
Hayo yamezungumzwa na Mtafiti Mwanafunzi
wa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Frank
Rwegoshora alipokuwa akiwasilisha sehemu ya matokeo ya Utafiti wake wa
miaka minne aliyokuwa akifanya juu ya kemikali zilizopo kwenye mimea dawa
kulingana na mazingira ya kijiografia na umri wa mmea dawa husika.
Mtafiti huyo amesema
waganga wengi wa tiba asili hapo awali walikuwa hawafahamu kuwa mimea dawa ina
kemikali na kwamba kemikali hizo ndizo zinazotibu magonjwa na kwa namna hiyo
lazima watambue kiasi cha dawa ambacho mgonjwa anapaswa kupewa ili dawa
zisilete madhara au kushindwa kutibu kutokana na kumpa mgonjwa dozi ndogo au kubwa..
Rwegoshora
amesema kuwa utafiti wake ulijikita kwenye mmea dawa wa Mvunjakongwa “Synadenium glaucescens Pax” unaopatikana
maeneo mengi ya Tanzania.
“Mimea inazo kemikali nyingi na una sehemu mbalimbali kama vile mizizi, majani na magome ambazo zinatumika kutibu, na mimi utafiti wangu unahusika na kemikali za mmea huu lengo kubwa ni kuanisha kemikali zilizomo kwa mtiririko wa namna gani na umri wa mmea huu wa Mvunjakongwa ili tusije jikuta tunavuna ile miti iliyokomaa peke yake kumbe tungeweza kupata matokeo mazuri hata kwenye ile miti midogo”, alisema Rwegoshora.
Watafiti
wakifanya vipimo vya sampuli walizokusanya
Akielezea utafiti huo ambao umehusisha Mvunjakongwa
kutoka mikoa ya Njombe, Morogoro na Tanga amesema kuwa utafiti wake umevumbua
kemikali mpya kabisa duniani pamoja
na nyinginezo nyingi hadi ngazi ya
maumbo kamili (‘chemical structures’).
Kwa marejeo ya tafiti nyingine duniani amesema kuwa
mmeo huo kemikali zake zinaweza kuondoa sumu mwilini pamoja na kufanya vizuri
kwenye magonjwa ya kansa mbalimbali pamoja na kisukari.
Aidha amewataka wananchi kuwa na subira juu ya matokeo
hayo ya tafiti na kwamba wasianze kuvuna na kuuza dawa moja kwa moja wasubiri
matokeo ya kina juu ya mmea huo.
“Tumeweza kugundua kemikali nyingine mpya kabisa
ambayo haijawahi gundulika kokote duniani ambapo awali ziligundulika kemikali
nne tu lakini kwa sasa kipo kilichoongezeka ambacho ni sifa pia kwa nchi yetu”,
alisema Rwegoshora.
Aidha Rwegoshora ameongeza kuwa taarifa nyingine
zilizopo juu ya mimea hiyo huwa wanatumia kwaajili ya kutibu mafindo findo ya
ng’ombe, virusi vya ukimwi (VVU), kifua kikuu na kikohozi kikali, kuzungushia
kwenye ghara ya nafaka kwa ajili ya kuzuia vijidudu, kutibu tumbo ambapo huchanganywa
na vitu kama asali, pamoja na kutibu matumbo ya hedhi kwa wanawake.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili
na Tiba Mbadala Prof. Hamisi Malebo amepongeza kazi kubwa ya utafiti inayofanywa
na watafiti kutoka SUA na kwamba tafiti zao zinasaidia katika kuboresha namna
wataalamu wa tiba asili wanavyoweza kutoa tiba kisayansi.
1.
Mwenyekiti
wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Prof. Hamisi Malebo akizungumza na wadau hawapo pichani katika mawasilisho ya utafiti
“Mradi huu wa GRILI umefanya kazi kubwa sana katika
kuboresha kazi za waganga wa tiba asili nchini katika maeneo mbalimbali ya
ufungashaji, usindikaji wa bidhaa zao na masuala muhimu ya masoko ili waweze
kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa”,alisema Prof. Malebo.
Prof. Malebo amewataka watafiti na taasisi za utafiti
nchini kufanya utafiti wa kina ili kuleta matokeo ya kisayansi kwani kwa sasa
kumekuwa na mwamko mkubwa wa jamii katika matumizi ya dawa za asili hivyo ni
lazima sayansi itumike katika kupata majibu sahihi ya matumizi ya mimea dawa
nchini na kama zinavyofanya nchi zingine kama vile India na China na kunufaisha
jamii na taifa.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala amesema Baraza hilo tayari limesajili dawa za asili ambazo zinaonesha
uwezo mkubwa wa kupambana na Virusi vya Ukimwi na ambazo pia zinaonesha uwezo
wa kuinua afya na kinga za watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Mradi wa Utafiti wa Kuongeza Ubunifu katika Mimea dawa
ili kuboresha Maisha (GRILI) ulianza
mwaka 2010 na unawashirikisha wadau mbalimbali kama vile Chuo Kikuu cha SUA,
Mzumbe, Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Taasisi ya Dawa Asili
Muhimbili (ITM) na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA)
Wadau wengine ni Taasisi ya Utafiti wa Dawa za
Binadamu (NIMRI), Chuo Kikuu cha Sayansi Nelson Mandela(NMIST), Shirika la
Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) pamoja na Waganga wa tiba
asili na watumiaji wa mimea madawa
nchini kwa ufadhili wa shirika la maendeleo la Denmark DANIDA.
0 Comments