SUAMEDIA

TPRA inamchango mkubwa katika kudhibiti na kutokomeza visumbufu mazao - Prof. Sibuga

 

Na Gladness Mphuru

SUA

Imeelezwa kuwa Taasisi ya Kuhakiki Viuatilifu (TPRA) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki inamchango mkubwa katika kudhibiti na kutokomeza visumbufu mazao, kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hususani pamba, kahawa, mbogamboga na hivyo kuleta tija kwa wakulima.


Prof. Pilly Sibuga akitoa Mada yake katika Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Jijini Mwanza (Picha zote na Gerald Lwomile)

Hayo yameelewa hivi karibuni na Prof. Kalunde Pilly Sibuga kutoka Idara ya Sayansi ya Mazao na Kilimo cha Bustani kutoka SUA mkoani Mwanza, kwenye Kongamano la Kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru, ambalo limeshirikisha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia na mwenyeji Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT).

Prof. Sibuga amesema upatikanaji wa viuatilifu vilivyosajiliwa kihalali na TPRA vimeongezeka na kuwarahisishia watumiaji ambao ni wakulima upatikanaji kwa urahisi, licha ya kwamba kwa sasa wanaendelea kufanya jitihada za kuvumbua viuatilifu vya kibaiolojia ambavyo havitakuwa na sumu inayosababisha madhara kwa afya za binadamu pamoja na viumbe hai wengine.

“Kumejitokeza visumbufu vipya kwa mfano viwavi jeshi vamizi, kumejitokeza nzi wa matunda, ambao wameharibu matunda yetu na mboga zimeshindwa kupata soko la kimataifa, kumejitokeza magugu vamizi katika maeneo ya malisho, katika maeneo ya mashamba  na katika mbuga za wanyama kwahiyo hizi zote ni changamoto na inabidi tuzishughulikie”

Akizungumzia matumizi teknolojia za kilimo Prof. Sibuga amesema bado asilimia kubwa ya wakulima wa Tanzania wanatumia zana duni za kilimo kama jembe la mkono huku wanaotumia mashine kama trekta na pawatila ni wachache na ameongeza kuwa mpaka mwaka 1985 kulikuwa na matrekta 18,500 tu.


Washiriki wa Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru wakisikiliza Mada kutoka kwa Prof. Sibuga

Aidha sambamba na hilo amesema teknolojia katika uzalishaji wa vitalu nyumba umeanza kukua katika miaka mitano iliyopita na kimekuwa kivutio kikubwa kwa vijana kujihusisha na kilimo licha ya kuwa na changamoto ya gharama, uelewa kuwa chini na hivyo kutoa fursa kwa vyuo vya kilimo.

“Kilimo cha vitalu nyumba kimekuwa kivutio kikubwa kwa vijana kuingia katika kilimo kwa sababu unaweza kufanya uzalishaji mkubwa kwenye eneo dogo, anaweza kuzalisha mwaka mzima na anaweza kurudia mara kadhaa na vimekuwa, kwa mfano Chuo cha Sokoine kimeingia makubaliano na shirika lisilo la kiserikali ili kuwawezesha vijana kupata uzoefu katika kilimo hiki kwa hiyo haya ni maendeleo na vijana wengi wamevutiwa”

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo Mhe. Paul Kimiti, amesema amekuwa akikipenda kilimo tangu enzi za utoto wake katika utawala wa wakokoloni, hadi kufikia kuwa Mkuu wa Vyuo vya Kilimo na hata Waziri wa Kilimo, kadhalika amehusisha Siasa na Kilimo na kurejea machapisho ya kitabu alicho kiandika mwaka 1971 kiitwacho (Siasa Tano katika Kilimo).

Kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa “Mchango wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya Tanzania: Mafanikio na Changamoto Miaka 60 baada ya Uhuru”.

Post a Comment

0 Comments