SUAMEDIA

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imewataka wanafunzi wasio wanachama wa SUGECO kujiunga na chama hicho

 

Na. Ayoub Mwigune

SUA

Afisa Ushirika toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Esther Kisiga, amewataka wanafunzi ambao sio wanachama wa SUGECO yaani (Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative) kujiunga na chama hicho ili kupata manufaa  kwenye mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kuwekeza, uongezaji wa hisa kwa wanachama ili kukuza mtaji.

          

Afisa Ushirika toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Esther Kisiga akizungumza katika Mkutano Mkuu wa SUGECO

Bi. Kisiga ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa SUGECO uliofanyika Alhamisi Tarehe 9 Disemba, 2021 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro.

Amesema mkutano huo umekuwa ni wa amani na wa faida kubwa kwa wanachama, hususani katika suala zima la kukubaliana kwa pamoja katika kutatua changamoto mbalimbali za kilimo, kumuinua mkulima ambae ni mwanachama kiuchumi pamoja na kupanga mikakati kwa miaka mitano ijayo kwa kuanza na kuanzisha huduma za ugani kibiashara.

Aidha, akitoa pongezi kwa   chama hicho Bi.Kisiga amesema kuwa SUGECO imepanga kuwakodishia  mashamba wanachama wao, kwa ajili ya kukuza kilimo biashara ili kuinua uchumi wa mtu binafsi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUGECO, Bw. Revocatus Kimario, amesema moja kati ya mambo yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuanzisha mpango mkakati wa SUGECO kwa miaka mitano.

Kimario ametaja mambo watakayoanza nayo ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa huduma za ugani kibiashara ili kuhakikisha kwamba  wanachangia juhudi za Serikali katika kuhakikisha huduma hizo zinazotoka kwa wataalamu ili wakulima wazipate kwa wakati

Sisi kama SUGECO tunataka kushiriki kama sehemu ya kuandaa wataalamu ambao wataenda kutoa huduma za ugani kibiashara na hii tunataka kutumia vijana wetu waliopata nafasi ya kupata mafunzo nje ya nchi hususani Israeli na Marekani wanaporudi kuweza kushirikisha na kutumia maarifa waliyo nayo katika kuwatengeneza wenzao na kwenda kwa wakulima­.. amesema Revocatus Kimario.

Ameongeza kuwa huduma za Ugani kwa wakulima zitaenda kutolewa kwa mazao tofauti tofauti kulingana na maeneo yaliyopo kwa kuanza na mazao ya bustani kama kahawa, korosho,maharage na mahindi ili kusaidia wakulima kuweza kuzalisha kwa tija, kuongeza kipato, pamoja na kutengeneza ajira lengo likiwa ni kuisaidia Serikali katika kutatua changamoto ya ajira nchini.

Naye, Meneja Mwendeshaji SUGECO, Bw. Joseph Masimba, amesema Mkutano Mkuu wa Mwaka ambao umeambatana na Taasisi ya chama hicho imefikisha miaka 10 ambapo, taasisi  imekuwa katika  kutoa huduma, kuatamia pamoja na ujuzi kwa vijana ambao umekuwa unapelekea vijana kujitengenezea ajira mbalimbali nchini.


Baadhi ya waanzilishi wa SUGECO waliotunikiwa  vyeti ikiwa ni sehemu ya kutambua uanzilishi na na ukuaji wa ushirika huo

Pia Bw.Masimba, amesema kuwa kwa sasa SUGECO imekuja  na  mradi wa Kizimba Business Model ambao wameuzindua mwezi march  ambapo kupitia mradi  huo  watachukua eneo kubwa la ardhi watakaloliendeleza na kutengeneza mazingira na miundo mbinu yake kwa ujumla.

Ameongeza kuwa SUGECO imepanga  kuwatengenezea  vijana mazingira mazuri ya kupanga   katika eneo hilo, huku ikiwa na jukumu la kusimamia  upatikanaji wa masoko ili kijana aliyepanga katika eneo hilo afaidike.

Katika Mkutano huo Mkuu, Waanzilishi wa SUGECO wametunukiwa vyeti ikiwa ni sehemu ya kutambua uanzilishi na ukuaji wa ushirika huo  na mpaka sasa imefikisha miaka kumi tangu kuasisiwa kwake.

     Wanachamama SUGECO wakifuatilia  Mkutano Mkuu wa SUGECO 

Post a Comment

0 Comments