Calvine Gwabara.
Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia kitengo cha
SUA Innovation Hub, kwa kushirikiana na kampuni ya AQUILA EYES GROUP (AEG) ya
Morogoro nchini Tanzania kwa udhamini wa “The Belt and Road Geospatial
Information Training Center (BRGTC)” wamefanikiwa kuendesha mafunzo ya siku
tatu ya kimataifa ya matumizi ya mifumo ya taarifa za Kijographia (GEOSPATIAL INFORMATION SCIENCE) katika
kutambua na kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji wa taarifa na matumizi
yake katika sekta mbalimbali nchini.
Pichani ni washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya kimataifa ya matumizi ya mifumo ya taarifa za Kijographia
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa shahada za juu, utafiti
uhaulishaji wa Teknolojia na ushauri wa kitaalamu Dkt.Aquilina Mwanry
amepongeza jitihada kubwa zilizofanywa na wadau hao na kufikia hatua ya kuendesha
mafunzo hayo ya kwanza nchini, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),
Morogoro na kuomba SUA iwe kitovu/kituo ambacho kitasaidia kutoa mafunzo haya
kwa wadau mbalimbali katika matumizi ya teknolojia hiyo kwa kushirikiana na
mdau mwenza (AQUILA EYES GROUP).
“Nimefurahishwa kusikia kuwa kituo kinakuwa na malengo
mbalimbali ambayo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa taaluma mbalimbali zinazohusu
uchunguzi na maswala ya mifumo ya Sayansi ya kijografia (GIS) na ufafanuzi wa
picha za anga (satellite images) kwa wanataaluma, taasisi na sekta binafsi kwa
lengo la kuwaunganisha na kuhakikisha ushirikiano katika maswala ya Taarifa za
Jongrafia (GIS) lakini pia kubwa zaidi ni kutambua wadau katika matumizi ya Teknolojia
hii ikiwemo wanafunzi, taasisi binafasi na zile za kiserikali” Alisema Dkt.
Mwanri.
Ameongeza kutokana na umuhimu wa Teknolojia hiyo ameomba
waandaaji wa mafunzo hayo kuona sababu ya kuendesha mafunzo ya mara kwa mara
nchini ili kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi katika matumizi ya Teknolojia
hiyo ili iweze kurahisisha kazi zao na kuchochea uchumi wa taifa hasa
ikizingatiwa kuwa watu wengi hawaifahamu na hawatambui namna inavyoweza kurahisisha
kazi zao za kila siku kwenye taasisi zao.
Dkt. Mwanri amesema anatambua ukuaji mkubwa katika Teknolojia
za kijografia lakini bado nchini kuna changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na utaalamu,
mbinu na matumizi ya teknolojia kuwa machache, hivyo ni wakati sasa vijana
walio kwenye fani hizo kuchangamka na kutafuta elimu zaidi na za kisasa kwenye
maeneo hayo nchini.
“Mafunzo haya ya Teknolojia hii ya mfumo wa taarifa za kijiografia
(GIS) na ufafanuzi wa picha za anga (Remote Sensing) nchini ni muhimu sana
katika kuiunganisha Serikali na wadau lakini pia inagusa maswala ya Afya, majanga
kama mafuriko, tetemeko la ardhi, moto, uharibifu wa misitu, na mambo mengine mengi hivyo ni muhimu
kuendesha mafunzo haya mara kwa mara ambayo yatawezesha kuongeza ufanisi katika
kupata taarifa mbalimbali ambazo zipo kwenye mfumo huo kwa matumizi mbalimbali
ya kimaendeleo” Aliongeza Dkt. Mwanri.
Kwa upande wake Dkt. Doreen Ndossi ambaye ni Mratibu wa
uhaulishaji wa Teknolojia na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA amesema ni fursa
kubwa ambayo Chuo imeipata kupitia mkataba huo wa ushirikiano na wadau hao
ambao umefanikisha mafunzo hayo ambayo yanakwenda kusaidia kujenga uelewa kwa
wadau juu ya matumizi ya Teknolojia hiyo ya kisasa.
‘’Sisi kama Kurugenzi tunaona uwepo wa Teknolojia hiyo
utasaidia sana katika kutoa taarifa mbalimbali muhimu za kazi tunazofanya
Chuoni kwa wadau wetu mbalimbali na kufikia jamii kubwa zaidi na ndio msingi
hasa wa mkataba wa makubaliano (MoU) tuliyosaini ili kufanya kazi nao kwa
pamoja na kwa ukaribu kwa manufaa mapana ya Chuo na Taifa letu” Alibainisha
Dkt. Ndosi.
Awali Mratibu wa mafunzo hayo nchini Dkt. Neema Sumari amesema
kuwa wanafanya mafunzo hayo kwa kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali wa sekta
binafsi na za kiserikali ili kuweza kuwafundisha namna ya kutumia mfumo huo wa
kisasa ili waweze kwenda kuutumia na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
“Kwa kutumia mfumo huo utasaidia kupunguza gharama na muda
katika kupata taarifa mbalimbali za kila sekta kulingana na mahitaji yao na
kupitia mkataba wa makubaliano (MoU) kati ya SUA na iSpatial wanaweza kupata
taarifa na elimu muhimu wanazohitaji kwa urahisi tofauti na sasa” Alibainisha
Dkt. Sumari.
Dkt. Sumari amesema kwa mwaka huu ushirikiano huo umefanyika katika
nchi mbili za Afrika ikiwemo Afrika ya kusini na Tanzania, na tayari mafunzo
kwenye nchi hizo yamefanyika. Ambapo kila nchi imechagua mada kuu ya mafunzo,
kwa kulingana na mahitaji ya taasisi mbali mbali kwa wakati huo.
Mafunzo hayo ya kwanza nchini ambayo ni ya siku tatu
yanayowakutanisha wadau kutoka mashirika na taasisi za Serikali na zisizo za
kiserikali yamefadhiliwa na BRGTC na kuandaliwa
na SUA pamoja na kampuni ya AQUILA EYES
GROUP kwa uratibu wa kitengo cha SUA
Innovation Hub.
0 Comments