Na Hadija Zahoro
SUA
Mhadhiri Mwandamizi kutokea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
SUA Prof. Dominic Kambarage, amezishauri taasisi zinazohusika na sekta ya
mifugo, kuanzisha mikakati ya kitaifa ya kuhakikisha vijana wanaomaliza elimu
katika ngazi mbalimbali, kujiajiri hadi kufikia hatua ya kuajiri wengine.
Prof. Kambarage
Prof. Kambarage ametoa kauli hiyo wakati wa kongamano la
kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru katika Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Augustino (SAUT)
jijini Mwanza na kubeba kauli mbiu isemayo ‘Mchango wa Sekta ya Kilimo katika
Maendeleo ya Tanzania: Mafanikio na Changamoto Miaka 60 Baada ya Uhuru’.
Amesema sekta ya mifugo inahitaji kufikiriwa zaidi ili
iweze kusonga mbele, kwasababu mfuko wa
uwezeshaji wa kiuchumi ulioko
Halmashauri nchini haujafanya kazi vizuri ilihali, asilimia kubwa ya mapato
yake inagawiwa katika makundi mbalimbali yakiwemo, walemavu asilimia 20% wakina
mama asilimia 40% na vijana asilimia
40%.
“Sekta ya mifugo ni moja ya sekta ambazo mtu anaweza kujiajiri na kuajiri
wengine, mimi niombe tu SUA na Wizara
zinazohusika pamoja na watu wengine tuwe na mikakati ya kitaifa kuona jinsi gani vijana wanawezaje kuajiriwa na kuajiri
wengine, kwasababu mfuko wa uwezeshaji wa kiuchumi ulioko katika Halmashauri haujafanya kazi
vizuri sana, hivyo tunahitaji kuifikiria sekta hii ili tusonge mbele “.Amesema Prof. Kambarage.
Ameongeza kuwa idara ya maziwa na nyama pekee, haina uwezo wa
kutoa fursa pana za ajira hivyo, vijana wapewe fursa hizo katika sekta ya
mifugo, kilimo, uvuvi pamoja na sekta ya uzalishaji ili ziwasaidie kukuza
uchumi wao pamoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha, akitaja idadi ya ng’ombe iliyopo nchini, Prof.
kambarage amesema Tanzania ina asilimia
11% ya ng’ombe wote waliopo Afrika na
1.7% ya ngombe kwa ulimwengu mzima.
Ameeleza kuwa katika kaya zilizopo vijijini, ni kaya milioni
4.6 zinajihusisha na ufugaji, ambapo ni asilimia 50% ya kaya zote zilizopo
nchini kote, idadi ambayo ni ndogo katika kuchangia pato la Taifa.
Prof.Kambarage ameongeza kuwa
badala ya kununua ng’ombe kutoka nchi nyingine kama vile Afrika Kusini, Tanzania
inatakiwa kuwa na uzalishaji wa ng’ombe bora kwa sababu ina wataalamu wengi
kutokea ngazi ya elimu ya uzamivu (PhD),
ambao wana uwezo wa kuzalisha mifugo mizuri kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi
ambapo tangu 2016 mpango huo ulikuwepo, lakini mpaka sasa haujafanyiwa kazi yoyote.
“Nchi hii tuna mifugo, lakini hatuna mifugo bora, ukisikia mtu ana mifugo
mingi bora, ujue amenunua Afrika ya Kusini au Kenya sasa inakuwaje nchi kama
hii ina wataalamu wenye PhD, tunashindwa kuwa na koo safi na mali nzuri, mimi
naamini tuna uwezo wa kuwa na mifugo mizuri na kuisambaza kwa wananchi ” amesema Prof. Kambarage.
Ngongamano hilo la Maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru
lililokuwa limeshirikisha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu
cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, na mwenyeji Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT), limelenga tathmini ya maendeleo ya
nchi katika sekta mbalimbali tangu kupata uhuru wake mwaka 1961 mpaka sasa.
0 Comments