SUAMEDIA

Wanaharakati wa Rwanda washinikiza kufutwa kwa tamasha la Koffi Olomidé

Kundi la wanaharakati wa Rwanda wamedai kufutwa kwa tamasha la mwanamuziki wa Congo Koffi Olomidé lililopangwa siku ya Jumamosi katika mji mkuu, Kigali.



Wanataja sababu ni hukumu dhidi ya mwanamuziki huyo mwaka wa 2019 na mahakama nchini Ufaransa kwa ubakaji wa mmoja wa wanenguaji wake wa zamani alipokuwa na umri wa miaka 15, miongoni mwa makosa mengine.

Katika taarifa, wanaharakati hao walisema kumruhusu nyota huyo wa Congo kutumbuiza kwenye tamasha hilo "kunakiuka ahadi ambazo Rwanda imeweka kufikia usawa wa kijinsia na kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana".

Kundi hilo linaundwa na mashirika 29 yanayoshiriki katika kampeni dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Rwanda.

Koffi ni nyota mkubwa wa rumba na soukous ambayo ni maarufu kote barani Afrika.

Amekuwa matatani mara kadhaa hapo awali, ikiwa ni pamoja na kumpiga mcheza densi wake mmoja nchini Kenya mnamo 2016 na kudaiwa kumpiga mpiga picha nchini Zambia mnamo 2018.

Koffi Olomide: Tutarajie nini kwenye kesi ya unyanyasaji wa kingono, ubakaji inayomkabili?

Post a Comment

0 Comments