- Ivana Davidovic
- Business reporter, BBC News
Maria anasema alikulia katika familia ya Kikatoliki "iliyokuwa na upendo" kwenye pwani ya mashariki ya Marekani na chakula kikuu cha Jumapili kilikuwa jambo la kila wiki.
Wazazi wake walikuwa na ndoa nzuri na alitaka heshima na ukaribu huo katika uhusiano wake mwenyewe.
Alipokutana na mumewe katika miaka yake ya ishirini, ilionekana kama mapenzi.
Lakini mapenzi yaliharibika haraka, na kugeukia hadithi ya miaka 25 ya unyanyasaji na udhibiti. Kwanza kulikuwa na kila aina ya majina. Kisha, udhibiti kamili wa fedha zake, mienendo yake, na hatimaye juu ya wana wao watatu.
Mumewe alimpinga kuwa na kazi ambapo atatangamana na watu wengine na akampiga marufuku kutumia kompyuta.
"Aliniita mnene kila siku, alikuwa akinizuia nitoke nyumbani akiwa na hasira" anakumbuka.
Hatimaye, matumizi mabaya ya fedha yaliongezeka. Kwanza, angemwondolea malipo yake kwenye kazi yake ya kusafisha, kisha, akaomba kadi za mkopo kwa jina la Maria kwa kutumia nambari yake ya kijamii.
Miaka sita iliyopita, hatimaye Maria alivunjika moyo alipomsikia akisema alitaka auawe. Kwa usaidizi wa kanisa na familia yake polepole aliandaa mpango wa kutoroka.
Baada ya kupoteza mali yao kwa kunyang'anywa, hatimaye alihamia kwa dada yake. Alipata kompyuta ya mkononi kwa mara ya kwanza na hatimaye akawa na uhuru wa kuanzisha akaunti ya Facebook. Alianza kuchumbiana.
Lakini muda mfupi baadaye, mume wake wa zamani angenukuu jumbe zake kwa mwanamume ambaye alikuwa akimwona. Mume wake wa zamani pia alianza kujitokeza popote alipokuwa.
Angemuona ghafla akiendesha gari nyuma yake kwenye barabara kuu. Wakati mmoja, aliogopa sana kwamba alikuwa akimfuata na angeweza kumtolea bunduki, hivi kwamba aliita polisi.
Ingawa hakushtaki, uwindaji huo ulipungua na akasonga mbali zaidi. Lakini aligundua kuwa alikuwa mwathirika wa kinachojulikana kama 'stalkerware'.
Stalkerware ni programu inayopatikana kibiashara ambayo hutumiwa kupeleleza mtu mwingine kupitia kifaa chake - kwa kawaida simu - bila idhini yake.
Inaweza kumruhusu mtumiaji kuona ujumbe wa mtu mwingine, eneo, picha, faili na hata kusikiliza mazungumzo yaliyo karibu na simu.
Ili kusaidia kutatua shida hii Eva Galperin aliunda Muungano dhidi ya Stalkerware mnamo 2019.
Aliamua kuanzisha kikundi hicho baada ya kuangalia ripoti kutoka kwa watu kadhaa wanaodaiwa kubakwa, ambao walikuwa na hofu kwamba maisha yao yanaweza kuendelea kuharibiwa na mnyanyasaji wao kwa kutumia teknolojia. Mtu anapoweza kufikia simu yako uwezekano wa mateso ni mkubwa, anaeleza. Kwa mfano mwathirika anaweza kudanganywa kwa vitisho vya kusambaza picha za karibu.
Bi Galperin anasema kwamba katika kesi za unyanyasaji wa nyumbani anazokumbana nazo, "kiwango fulani cha unyanyasaji unaowezeshwa na teknolojia kiko karibu kila mahali", na kwamba hii mara nyingi inajumuisha stalkerware.
"Mara nyingi inahusishwa na kesi za vurugu zaidi - kwa sababu ni chombo chenye nguvu sana cha udhibiti wa shuruti," anaongeza.
Utafiti unaonyesha kwamba kuenea kwa vifaa vya stalkerware ni tatizo linaloongezeka: Utafiti uliofanywa na Norton Labs uligundua kuwa idadi ya vifaa vinavyoonyesha kuwa vilisakinishwa iliongezeka kwa 63% kati ya Septemba 2020 na Mei 2021.
Ripoti yake ilipendekeza ongezeko hilo kubwa linaweza kuwa kwa sababu ya athari za marufuku ya kutotoka nje na watu kwa ujumla hutumia wakati mwingi nyumbani.
"Mali za kibinafsi zinaweza kufikiwa na watu kwa urahisi, na kuna uwezekano wa kuunda fursa zaidi kwa wahalifu wa unyanyasaji unaowezeshwa na teknolojia kusakinisha vifaa vya kuvinjari kwenye vifaa vya wenza wao," ripoti hiyo iligundua.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Bi Galperin ameweza kushawishi kundi la makampuni ya kupambana na virusi kuchukua aina hii ya programu hasidi kwa umakini zaidi, hii ilifuatia kusita kwa awali kuashiria stalkerware kama programu isiyotakikana - au programu hasidi - kwa sababu ya uwezekano wake kuwa halali katika matumizi.
Mnamo Oktoba, Google iliondoa matangazo kadhaa ya programu ambazo huwahimiza watumiaji watarajiwa kupeleleza simu za wenza wao. Programu hizi mara nyingi huuzwa kwa wazazi wanaotaka kufuatilia mienendo na ujumbe wa mtoto wao - lakini badala yake zimetumiwa tena na watumizi ili kuwapeleleza wenzi wao.
Moja ya programu hizo, SpyFone, ilipigwa marufuku na Tume ya Biashara ya Shirikisho la Marekani mnamo Septemba kwa kuvuna na kupeana data kuhusu mienendo na shughuli za watu kupitia udukuzi wa kifaa kilichofichwa.
Licha ya hatua hizi chanya, baadhi ya programu za stalkerware, na ushauri wa jinsi ya kuzitumia, bado zinapatikana kwa urahisi mtandaoni.
Kulingana na Bi Galperin, suala linalofuata ambalo FTC inachunguza ni makampuni yanayouza na kununua data ya eneo la simu za watumiaji bila wao kujua. Anaita teknolojia hii "zana yenye nguvu sana" kwa wachunguzi wa kibinafsi, ambao huitumia kufuatilia maeneo wanayolenga.
Pamoja na stalkerware iliyoundwa kimakusudi kuwa vigumu kuiona, hata wale ambao wana ujuzi zaidi wa teknolojia bado wanaweza kuwindwa nayo.
Mmoja wa watu kama hao alikuwa Charlotte (sio jina lake halisi), mchambuzi mkuu wa usalama wa mtandao.
Mara tu baada ya kuchumbiwa aligundua polepole mambo ya ajabu yalikuwa yameanza kutokea kwenye simu yake. Betri ingeisha haraka na simu yake ingezima na kuwashwa tena ghafla - ishara zote mbili za simulizi ambazo zinaweza kusakinishwa kwenye kifaa chake.
Ni mpaka mpenzi wake alipoweka wazi kuwa siku zote alikuwa anajua mahali alipokuwa, ndipo hatimaye aligundua kilichokuwa kikitendeka .
Ili kupata ushauri juu ya nini cha kufanya, alienda kwenye mkutano wa wadukuzi. Ilikuwa tasnia ambayo mwenzi wake alifanyia kazi na alikuwa akifahamu baadhi ya nyuso.
Alishtuka kugundua "utamaduni wa kukubali kuwa na uwezo wa kumfuatilia mwenzi wako".
Mazingira ya "tech bro" aliyokumbana nayo yalimchochea kuhamia usalama wa mtandao, ili kuimarisha "uwakilishi wa sekta hiyo kutoka kwa mitazamo tofauti".
Utafutaji wa haraka wa mtandao unaonyesha huduma nyingi zinazodai kuwa zinaweza kuingia kwenye simu ya mtu kwa kutumia nambari ya simu tu, kwa kawaida kwa dola mia chache za kulipwa kwa njia ya sarafu za kidijitali .
Hata hivyo, ingawa programu zilizo na uwezo huo zinaweza kupatikana kwa mashirika ya kutekeleza sheria, wataalamu wa usalama wa mtandao wanaamini kuwa huenda tovuti hizi ni za ulaghai. Badala yake, stalkerware ya kiwango cha watumiaji hutegemea sana "uhandisi wa kijamii," ambayo Charlotte anasema watu wanaweza kujifunza kuwa waangalifu.
Mtu anayelengwa anaweza kutumwa ujumbe wa maandishi, ambao unaonekana kuwa sawa, ukiwaalika kubofya kiungo.
Au programu ghushi, inayojifanya kuwa halali, mtu anaweza kuwatumia.
Charlotte anasema "usiogope" ukijaribu kufuta programu inayotiliwa shaka na inatoa onyo nyingi.
"Wakati mwingine hutumia mbinu za kutisha ili kuwafanya watumiaji wasiondoe programu. Wanatumia mbinu nyingi za uhandisi wa kijamii."
Ikiwa yote mengine hayatafaulu, Charlotte anapendekeza urejeshe mipangilio ya mwanzo ya simu yako, kubadilisha nywila zako zote za akaunti ya mitandao ya kijamii na kutumia uthibitishaji wa hatua mbili kila wakati unapoingia katika akaunti zako .
Kwa hivyo, ni ipi njia bora zaidi ya kushughulikia shida hii?
Nchi nyingi tayari zina aina fulani ya sheria ya kuzuia kudukuliwa kwa simu yako na sheria za kuzuia kunyatia.
Kwa mfano, mwaka wa 2020, Ufaransa iliwasilisha mswada mpya kuhusu unyanyasaji wa nyumbani ambao, miongoni mwa mengine, uliimarisha vikwazo kwa ufuatiliaji wa siri: kufuatilia mtu kujua aliko kupitia simu au chombo cha elektoniki- bila ridhaa yake sasa kunaadhibiwa kwa kifungo cha mwaka mmoja na faini ya €45,000 (£38,000; $51,000) ) Ikiwa hii itafanywa na mpenzi wako, faini zinaweza kuwa kubwa zaidi.
Njia za kusonga mbele
Lakini, kwa Eva Galperin, hili si tatizo ambalo tunaweza kutarajia sheria mpya kutatua kabisa.
Anafikiri kwamba Google na Apple zinaweza, kwa mfano, kuchukua hatua kwa kufanya isiwezekane kununua mojawapo ya programu hizi kwenye maduka yao.
Muhimu zaidi, anaongeza, lengo linapaswa kuwa katika mafunzo bora ili polisi wachukue tatizo kwa uzito zaidi.
Kuongezeka kwa unyanyasaji wa mtandao pia kumeleta aina mpya ya huduma kusaidia waathiriwa wa unyanyasaji wa nyumbani.
Kliniki ya Kukomesha Unyanyasaji wa Kiteknolojia - CETA - ni mojawapo ya vituo hivyo, vinavyohusishwa na Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani. CETA hufanya kazi moja kwa moja na walionusurika na unyanyasaji, wakati huo huo inakusanya utafiti kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia yanayochipuka.
Rosanna Bellini kutoka CETA anasema kwamba mara kwa mara wanaweza wasipendekeze kuondoa vifaa vya kuogofya kutoka kwa simu ya mwathiriwa mara moja - bila kupanga mipango ya usalama kwanza na mfanyakazi nayeshughulikia kesi. Uzoefu wa waliyopitia zamani umesababisha kutumiwa kwa mbinu hii: ikiwa ufikiaji wa mnyanyasaji kwa simu ya mwathiriwa unakatwa ghafla, inaweza kusababisha kuongezeka kwa vurugu.
Kwa Maria, ambaye amekuwa huru kutoka kwa ndoa yake yenye unyanyasaji kwa miaka sita, mambo si mazuri lakini yanaelekea huko.
"Niko kwenye uhusiano mzuri na mtu ambaye ananijali sana na yuko nyuma yangu, akisimulia kisa changu," anasema.
Bado kuna nyakati anapata wasiwasi kuhusu simu yake. Aligunduliwa na ugonjwa wa (PTSD). Lakini anataka manusura wengine wajue kwamba ufuatiliaji wa mtandao ni jambo kubwa na kwamba hawako peke yao.
"Usiogope. Kuna msaada huko nje. Nimepiga hatua kubwa na kama naweza kufanya hivyo katika umri wangu - wa miaka 56 - mtu yeyote anaweza kufanya hivyo."
0 Comments