SUAMEDIA

Omicron:Biden akaza masharti ya usafiri huku Ujerumani ikiwafungia watu ambao hawajachanjwa

 Rais Joe Biden amezindua masharti makali ya usafiri kukabiliana na Covid-19 huku Amerika ikithibitisha visa vingi vya aina mpya ya kirusi cha Omicron kutoka pwani hadi pwani.

Bw Biden alisema mpango wake "haujumuishi kufungwa au zuio la kutoka nje " na haupanui maagizo ya kutakiwa kuchanjwa.

Visa vimegunduliwa huko California, Colorado, Minnesota, New York na Hawaii, ambapo maafisa wanasema mtu huyo hakuwa na historia ya hivi majuzi ya kusafiri.

Maafisa wa afya wa eneo hilo wameripoti dalili ndogo tu katika visa hivyo.

Aina hiyo ya kirusi sasa imepatikana hadi nchi 30, kulingana na ripoti.

Bado haijabainika ikiwa aina ya Omicron inayobadilika sana inahusishwa na maambukizi zaidi au hatari zaidi ya kukwepa chanjo.

Mpango wa Biden ni upi?

Chini ya maelezo yaliyozinduliwa Alhamisi, abiria wote wa kimataifa watalazimika kupimwa virusi ndani ya saa 24 kabla ya kuondoka kwenda Amerika, bila kujali hali yao ya chanjo. Mahitaji ya barakoa kwenye ndege, treni na mabasi yataongezwa hadi Machi.

Serikali ya Marekani italenga kutoa mamilioni ya vipimo vya bure nyumbani kupitia kampuni za bima za kibinafsi kwa wale ambao wana bima na kupitia vituo vya afya na kliniki za vijijini kwa wale ambao hawana.

Mpango wa utawala wa miezi ya msimu wa baridi pia una hatua za kuwahimiza watu wazima wote kupata chanjo zao za nyongeza, ikijumuisha kupitia kampeni ya elimu kwa umma na uhamasishaji unaolengwa zaidi.

Zaidi ya Wamarekani milioni 40 wamepokea chanjo za nyongeza, lakini Bw Biden alisema karibu milioni 100 zaidi wanastahiki na bado hawajapata zao.

Mamia ya kliniki za kifamilia za chanjo zitaanzishwa kote nchini katika jaribio la kuongeza viwango vya chanjo miongoni mwa watoto na vijana.

Marekani na mataifa mengine kadhaa yamepiga marufuku kusafiri kutoka nchi nane za kusini mwa Afrika. Wataalamu wa afya wamesema vikwazo vya usafiri vitawapa muda wa kusoma na kuifanya utafiti zaidi aina hiyo mpya ya kirusi

Ujerumani yachukua hatua

Viongozi wa kitaifa na wa kikanda wa Ujerumani wamekubali kuwazuia watu ambao hawajachanjwa kushiriki pakubwa katika maisha ya umma kwa nia ya kuzuia wimbi la nne la Covid-19.

Kansela anayemaliza muda wake Angela Merkel alielezea hatua hizo kubwa kama kitendo cha "mshikamano wa kitaifa".

th

CHANZO CHA PICHA,AFP

Ni wale tu ambao wamechanjwa au kupona hivi majuzi kutokana na Covid ndio watakaoruhusiwa katika mikahawa, sinema, maeneo ya starehe na maduka mengi.

Chanjo zinaweza kufanywa kuwa za lazima ifikapo Februari, kansela aliongeza.

Wimbi la nne la Covid-19 la Ujerumani ndio kali zaidi hadi sasa, na vifo vingine 388 vilirekodiwa katika saa 24 zilizopita.

Pia kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya kuenea kwa Omicron, ambayo maafisa wa afya wa EU wanaonya kuwa kunaweza kusababisha zaidi ya nusu ya kesi zote za Covid katika miezi michache ijayo.

Bi Merkel alisema hospitali zimezidiwa hadi wagonjwa kulazimika kuhamishwa hadi maeneo tofauti kwa matibabu. "Wimbi la nne lazima livunjwe na hii bado haijapatikana."

"Kutokana na hali hiyo, nadhani inafaa kupitisha sheria ya chanjo ya lazima," alisema, huku akiweka wazi kwamba hii itabidi kuidhinishwa na bunge.


ChanzoBBC Swahili

Post a Comment

0 Comments