Na.Vedasto George
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan ameyataka Mashirika na Taasisi za kidini nchini kuwa na uwazi wa taarifa
na mahesabu yao ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazo jitokeza pindi serikali inapotaka kukusanya kodi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba yake katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Jumuhiya ya Kikristo ambao umefanyika Kilakala Mkoani Morogoro.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 8 katika Mkutano
Mkuu wa 31 wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania CCT Mjini Morogoro na kusema kuwa serikali inalazimika kuyatoza kodi
mashirika ya kidini kutokana na baadhi ya taasisi hizo kuwa na mazingira ya
kibiashara na sio kihuduma.
Aidha Mhe. Samia amesema serikali itaendelea kuheshimu misingi
ya utawala wa sheria na haki za binadamu na kuongeza kuwa haitasita kuchukua
hatua kali kwa viongozi na watendaji wa serikali wasio heshimu utawala bora na
kukiuka haki za kibinadamu.
Awali akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa CCT Askofu
Dkt. Alinikisa Cheyo amesema miongoni mwa majukumu wanayofanya kwa kushirikiana
na taasisi mbalimbali na Serikali ni shughuli za kijamii zenye lengo la kuimarisha
haki, kujenga usawa wa kijinsia, na kuwajengea watu uwezo wa kuinua vipato vyao
ili kuweza kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Mchungaji Agines Njeyo Mwenyekiti wa wanawake wa
CCT ameoimba Serikali kufanya mabadiliko ya kisera, kisheria na utaratibu ambao
utawawezesha watoto wa kike nchini kurudi kwenye mfumo rasmi wa kielimu baada
ya kupata ujauzito.
Mkutano Mkuu wa 31 wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT umeambatana na Uchaguzi Mkuu wa kuwachagua
viongozi wapya wa Jumuiya hiyo ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka minne.
0 Comments