Shirika la Afya Duniani (WHO) limezitaka nchi za Kiafrika kutoharibu chanjo za Covid-19 ambazo zimepitisha muda wa matumizi
Nchi hizo zimeambiwa zihifadhi chanjo hizo na kusubiri mwongozo zaidi.
Ombi hilo linakuja baada ya Malawi na Sudan Kusini kusema zitaharibu zaidi ya dozi 70,000 za chanjo ya Oxford-AstraZeneca kwa sababu muda wa matumizi yake ulikamilika mwezi Aprili.
Lakini Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa (Africa CDC) kilisema kimehakikishiwa kuwa chanjo hiyo ni salama kutumiwa.
Chanjo nyingi zinaweza kutumiwa hadi miezi 36 baada ya utengenezaji, lakini kwa sababu chanjo za Covid-19 ni mpya sana hakuna data ya kutosha kuthibitisha ufanisi wao kwa muda mrefu.
Uamuzi wa mwisho juu ya kutumia chanjo zilizopitisha muda wake wa matumizi ni wa wasimamizi wa kitaifa wa dawa.Mwandishi wa BBC wa afya huko Nairobi, Rhoda Odhiambo, anabainisha.
Utoaji wa chanjo za coronavirus kote Afrika umekuwa polepole, kwa sababu ya maswala ya usambazaji na wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa chanjo hiyo
"Ombi langu kwa nchi wanachama ni: ikiwa tunafanya wajibu wetu wa kuhakikisha kuna chanjo hizi , fanyeni wajibu wenu na mtumie chanjo," John Nkengasong, mkurugenzi wa Afrika CDC, aliambia mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.
Malawi ilisema imepanga kuharibu zaidi ya dozi 16,000 za chanjo ya AstraZeneca, ambazo zilitengenezwa na Taasisi ya Serum ya India (SII), kwa sababu tarehe yao ya matumizi ilikuwa 13 Aprili.
Sudan Kusini, wakati huo huo, ilipanga kutupa dozi 59,000 kwa sababu hiyo hiyo.
Dozi za chanjo hiyo zilitolewa kwa nchi 13 za Kiafrika kupitia ushirikiano kati ya Jumuiya ya Afrika (AU) na kampuni ya mawasiliano ya MTN Group, Peter Mwai wa BBC kutoka ya Reality Check ameripoti.
AU ilinunua dozi milioni moja ya chanjo ya AstraZeneca kutoka Afrika Kusini, ambayo ilikuwa imeacha kutumia chanjo hiyo huku kukiwa na mashaka juu ya ufanisi wake dhidi ya aina mpya ya virusi hivyo ambayo ilikuwa imesambaa nchini.
Afrika CDC ilipeleka dozi hizo kwa nchi hiyo mwishoni mwa Machi, wiki chache kabla ya muda wake wa matumizi kumalizika
Bwana Nkengasong, ambaye aliita hali inayozingira utoaji wa chanjo hiyo "kuwa na changamoto kubwa", alisema SII ilikuwa imeshauri Afrika CDC kwamba "chanjo bado zinaweza kutumika hata baada ya miezi tisa".
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti alizitaka nchi "kuhifadhi chanjo hizi salama tunapoendelea kusoma na kujaribu kupata ushauri dhahiri ikiwa chanjo zinaweza kutumika kwa muda mrefu".
`Kando na Malawi na Sudan Kusini, WHO ilisema Ghana na Sierra Leone pia hazijatumia chanjo zao zote kutokana na kupita kwa tarehe ya matumizi yake.
Waziri wa afya wa Sierra Leone alisema nchi hiyo imebaki na karibu theluthi moja ya dozi walizopokea. "Ilibidi tushindane ili kuhakikisha kuwa tunapeana kipaumbele matumizi ya chanjo hizi," Austin Demby aliambia BBC.
Kati ya nchi 55 za Kiafrika, 41 wamefaidika na utoaji wa chanjo kupitia mpango wa kugawana chanjo ulimwenguni wa Covax. Saba bado hazijapokea awamu ya kwanza.
Mpango wa Covax unakusudia kuhakikisha chanjo zinatolewa kwa usawa kati ya mataifa yote, matajiri na maskini. Kufikia sasa, zaidi ya dozi milioni 38 za chanjo zimepelekwa kwa nchi 98.
Wataalam wa afya wanasema upatikanaji sawa wa chanjo ni muhimu kumaliza janga hilo.
0 Comments