SUAMEDIA

SUA kutoa mafunzo kwa watafiti chipukizi katika Uandikaji Machapisho na Miradi ya kiutafiti


Na.Vedasto George.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Mfuko maalum wa kusaidia Watafiti Wanataaluma Vijana kimetoa mafunzo ya siku nne kwa wanataaluma na watafiti chipukizi, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo katika uandikaji Machapisho na Miradi ya kiutafiti ambayo ina tija kwa Taifa.


Akizungumza katika mafunzo hayo Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA amesema kuwa Chuo kupitia mapato yake ya ndani kwa mwaka huu wa fedha kimetenga kiasi cha sh.500,000,000/=( milioni mia tano) kwa ajili ya kuwezesha tafiti ambazo zinatokana na watafiti wanataaluma vijana ili waweze kufanya kazi zao za kiutafiti.

"Kwa kuwa hawa ni watafiti wadogo ambao kwanza wanajifunza namna ya kuandika miradi, namna ya kuandika machapisho imeonekana ni muhimu sana tuwe na mafunzo ya kuwajengea uwezo ili maandishi au tafiti zao ziweze kuwa na tija na matokeo makubwa kwa nchi yetu, mafunzo haya yameendeshwa na wataalamu wa SUA wabobezi", alisema Prof.Kshaigili.

Aidha Prof. Kashaigili amesema kutokana na dhana potofu iliyopo ya kuwa tafiti haziwasaidii wananchi, sasa kupitia mfuko huo ulioanzishwa na SUA utasaidia kujibu changamoto na kujikita zaidi katika kufanya tafiti zitakazoleta manufaa kwa wananchi.

"Ni kweli kumekuwa na hisia ya muda mrefu sana kwamba tafiti nyingi zinazofanywa haziwasaidii wanajamii kwa kiasi kikubwa kwa sababu tafiti hizo zimekuwa zikilenga machapisho ya kawaida tu, lakini niseme kwamba hii Progamu tuliyoianzisha hapa SUA,  matarajio yetu ni makubwa sana na tafiti zitakazo fanyika sasa zitajikita katika kutatua matatizo ya wananchi", amesema Mratibu huyo.

Akifunga mafunzo hayo Prof. Samweli Kabote kwa niaba ya Prof. Maulid Mwatawala ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa SUA  upande wa Taaluma amesema kuwa mbali na pesa hizo hizo zilizotengwa na Chuo (Tsh. 500,000,000/=) ili kusaidia watafiti wanataaluma vijana bado Chuo kimepanga kuongeza ufadhili huo na kufikia sh. bilioni moja. 

Kwa upande wake Mhadhiri kutoka SUA Dkt. Nicholas Mwalukasa ambaye pia ni Mtafiti Kijana pamoja na kukishukuru Chuo cha SUA kwa kutoa mafunzo hayo pia amebainisha kuwa pamoja na kazi kubwa zinazofanywa na Wanataaluma katika Chuo hicho za kufundisha na kufanya utafiti lakini pia wanapaswa kutoa ushauri kwa wananchi kupitia tafiti wanazozifanya.

Wataalamu 19 kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wanatarajia kunufaika na Mfuko maalum wa kusaidia Watafiti Wanataaluma Vijana ambao watafanya tafiti zao sehemu mbalimbali nchini Tanzania.


 


Post a Comment

0 Comments