SUAMEDIA

TBS kuwajengea uwezo Maafisa wa Serikali Morogoro

 

Na.Vedasto George.

Shirika la Viwango Tanzania TBS limetoa mafunzo kwa Maafisa wa Serikali ngazi ya Halmashauri mjini Morogoro kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya Viwango na Uthibiti ubora  ili kuweza  kuwaandaa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo katika halmashauri zao ambao ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa mbalimbali za viwandani.



 Akizungumza katika mafunzo hayo Meneja wa Utafiti na Mafunzo wa TBS  Hamisi Mwanasala amesema mafunzo hayo yametolewa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Viwanda Prof. Kitila Mkumbo ambapo alilitaka Shirika hilo kutoa elimu kwa Maafisa wa Serikali ngazi ya Halmashauli nchi nzima ili waweze kuwa mabalozi na kutoa elimu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo juu masuala ya Viwango na Uthibiti ubora.

 

"Tumetoa mafunzo haya kwa Maafisa hawa ili wawe na uelewa juu ya masuala ya Viwango na Uthibiti ubora ambapo wao sasa wataenda kuwatumikia wazalishaji ambao ni wajasiriamali kwa ujumla", alisema Mwanasala.

 Amesema TBS imefanikiwa kuwa na ofisi katika Kanda lakini kutokana na jiografia ya nchi ilivyo ni vigumu kuwafikia wananchi kwa haraka na kwa muda sahihi ndio maana wamewaelimisha maafisa hao kama wawakilishi wa utoaji wa taarifa za masuala ya viwango na uthibiti ubora kwa wananchi wengine.

Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala mkoa wa Morogoro Emmanuel Kalobero amesema mkoa huo huna wafanyabiashara wengi wanaozalisha bidhaa za viwandani lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji wa bidhaa zisizo na ubora na kuwataka watumishi hao kutumia mafunzo hayo kuwaelimisha wafanyabiashara ili wazalishe bidhaa nyingi na zenye ubora ambazo zitatumiwa na walaji pasipo kupata madhara.

Baadhi ya washiriki akiwemo Afisa Afya halmashauri ya mji wa Ifakara Jafari Hamisi pamoja na Kaimu Afisa Kilimo halmashauri ya wilaya ya Mvomero Suzy Mazengo wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi na kuwasaidia wafanyabiashara katika uzalishaji wa bidhaa ambazo ni  bora na zenye kukidhi viwango TBS.

"Kuna wajasiriamali wale wadogowadogo ambao wanafanya kazi katika ngazi zetu tutawapitia kuwaelimisha kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na ubora unaotakiwa unaolinda afya za watanzania lakini pia kuhakikisha wajasiriamali watapata soko la uhakikau", alisema Hamisi.

Mafunzo hayo yanayohusu masuala ya Viwango na Uthibiti ubora kwa Maafisa wa Serikali ngazi ya Halimashauri yametolewa mjini Morogoro yakishirikisha halmashauri zote za mkoa huo. 


Post a Comment

0 Comments