SUAMEDIA

Wakulima wa chai watakiwa kujengewa uwezo kwenye uzalishaji wa zao hilo

 

Na Amiri Kilagalila,Njombe.

Wakulima wa zao la chai hapa nchini wametakiwa kujengewa uwezo juu uzalishaji wa zao hilo na kuongeza thamani ili liweze kupata masoko ndani na nje ya nchi.





Kauli hiyo imetolewa  na Mratibu wa Mradi wa Markup Tanzania Safari Fungo katika kikao cha  kuwajengea uwezo wadau wa chai nchini kilichofanyika mkoani Njombe.

Mratibu huyo amesema  wazalishaji wa zao la chai wanapaswa kupatiwa mbinu na kujengewa uwezo kuanzia wakati wa kuvuna, kuongeza thamani pamoja na namna ya kupata masoko ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa  ili wakulima na wazalishaji wafanikiwe wanapaswa kupatiwa mafunzo ya nadharia kwa kujengewa uwezo darasani na baadae shambani kuona namna mafunzo waliyoyapata wanavyoweza kuyabadili katika vitendo.

Pia  mafunzo hayo yanaweza kufanikiwa na kuinua viwango vya ubora endapo wadau wa zao hilo wakiwemo viongozi kutoka serikalini na  wazalishaji wa zao hilo wadogo, wakati na wakubwa watashirikiana.

Amesema  hilo likifanyika zao hilo la chai kutoka Tanzania litaweza kupata masoko kuanzia ndani ya nchi na nje ya nchi hususani barani ulaya ambalo ndiyo wadhamini wa mradi huo.

"Ninaamini kupitia zoezi hili wakulima na wafanyabiashara watahakikisha mambo haya wanakwenda kuyatekeleza kwenye biashara zao" amesema  Safari.

 

 

Post a Comment

0 Comments