SUAMEDIA

Vyuo vyatakiwa kuongeza ufanisi katika kubuni na kutoa elimu itakayoleta maendeleo nchini

 

Na: Tatyana Celestine

Mkuu wa Idara ya Sera, Mipango na Menejimenti, Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Fatihiya Massawe amevishauri Vyuo na Taasisi mbalimbali kuhakikisha vinaongeza ufanisi katika kubuni na kutoa elimu itakayosaidia kuleta maendeleo nchini.


Akizungumza na SUAMEDIA April 19, 2021 ofisini kwake Prof. Fatihiya amesema kuwa SUA kwa kutambua mchango mkubwa inayotoa  kwa Taifa imeamua kujitanua na kuongeza Kozi mbalimbali zinazosaidia kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa lengo la kuongeza Wanataaluma wenye tija katika jamii.

Akizungumzia dhana ya watu kuona SUA inapaswa kutoa elimu ya Kilimo pekee, amesema kuwa yeye akiwa Mwanataaluma anaona ni vema  vyuo vyote duniani kuangalia namna ya kuunganisha taaluma mbalimbali ambazo zikitolewa vyuoni zitasaidia vijana kupata ajira na kutatua changamoto ambazo awali ilikuwa ngumu kuzitatua.

“Hapa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo tunatoa fani mbalimbali Mtambuka ikiwemo Mifugo, Kilimo, Misitu na Mazingira lakini tunayafanya yote haya ili kutoa wataalam ambao wanatakiwa kubadilisha maisha, kila kitu ambacho tunakifanya lengo ni kwamba tuyaone matokeo kwa mtu wa kawaida”, alisema Prof.Fatihiya.

Kuhusu umuhimu wa kozi mpya ya Mipango ya Maendeleo na Usimamizi ambayo ni mpya chuoni hapo, Mkuu huyo wa Idara amesema kuwa SUA ina kozi mbalimbali ambazo zinatolewa lakini kozi hiyo imewekwa kama kiungo kwa kozi nyingine itakayosaidia kutafsiri Maendeleo kwa mtu wa chini katika jamii.

Ameongeza kuwa wahitimu wa kozi hiyo wameonekana kuwa muhimu kwa kuwa wao ndio chachu ya kuunganisha wanataaluma wengine katika kozi mtambuka zinazotolewa chuoni hapo vivyo hivyo hufanywa hata katika vyuo vikuu duniani kwani kozi hiyo inakuwa kiungo katika tafiti zinazofanywa na Magwiji katika fani mbalimbali kuweza kuzitafsiri katika lugha ambayo mtu wa chini anaweza kuzitumia na kuleta tija.

“Ndio maana tunasema sisi ni Ndaki ya Kimkakati kuwepo ndani ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo inatusaidia kuwa kiungo kati ya watu hao wa Sayansi hizi (Hard science au Natural science) na Sayansi ya Jamii”, alisema Prof.Fatihiya.

“Sisi tunayo Degree hii ambayo inatoa Wataalam wa Mipango ya Maendeleo lakini pia watakaoweza kusimamia maendeleo, mtu anayesoma SUA na atakayesoma kwingine tofauti yake ni kupata kitu cha ziada, hapa atafundishwa masomo ya msingi kumfanya awe mtu wa mipango na usimamizi tena kuna kozi mbalimbali atapata faida ya kuzisoma”, alisema Prof.Fatihiya.

Kozi hiyo ya Mipango ya Maendeleo na Usimamizi imeanzishwa mwaka 2020/2021  na tayari wanafunzi 122 wanasoma kozi hiyo.

Post a Comment

0 Comments