SUAMEDIA

Majeshi ya Marekani kuondoka Afghanistan Septemba 11

 Rais wa Marekani Joe Biden ataviondoa vikosi vyote vya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan kabla kumbukumbu za miaka 20 za mashambulizi ya Septemba 11.




Hatua hii itakuwa imefikisha mwisho vita ilivyohusika Marekani kwa muda mrefu zaidi, licha ya hofu ya ushindi wa Taliban.

Kwa wiki kadhaa sasa Rais Biden amekuwa akionyesha ishara kwamba atauacha muda wa mwisho wa mwezi Mei, wa kuviondoa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, uliowekwa na mtangulizi wake Donald Trump upite.

Maafisa katika wizara ya ulinzi ya Marekani walikuwa wanaipinga tarehe ya mwisho ya kuondoa majeshi ya Mei mosi wakisema jambo hilo linastahili kufanyika kwa kuzingatia hali ya amani Afghanistan yakiwemo mashambulizi ya Taliban.


Marekani sasa kuwekeza raslimali zake kwa vitisho vinavyoikabili 

Kulingana na Katibu wa masuala ya waandishi wa habari katika ikulu ya White House Jen Psaki, hakuna cha ziada kinachoweza kuafikiwa Afghanistan na vikosi hivyo vitaanza kuondoka kuanzia Mei mosi. Psaki anasema Biden, atatoa tangazo rasmi kuhusiana na suala hilo Jumatano.

"Rais Biden anaendelea kudhamiria kuunga mkono majadiliano baina ya pande husika ambayo wengi wenu wanayafuatilia na ambayo yataanza tena wiki ijayo. Pia anaamini tunastahili kuwekeza raslimali zetu katika vitisho vinavyotukabili leo, karibu miaka ishirini baada ya kuanza kwa vita hivyo," alisema Psaki.

Chaguo la tarehe ya Septemba 11 kama siku ya mwisho ambayo vikosi vya Marekani vitakuwa vimeondolewa Afghanistan, linaonyesha sababu kuu iliyowapelekea wanajeshi hao kuwa nchini humo, kuyazuia makundi ya kigaidi kama al-Qaeda kutia guu Marekani na kufanya mashambulizi tena.

Psaki amesema wanajeshi wa Marekani watakaobaki katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ni wale watakaohusika n`a ulinzi wa wanadiplomasia tu.

Taliban kuususia mkutano wa kimataifa wa amani wa Uturuki

Hatua hii ya Rais Biden lakini, huenda ikapelekea wanamgambo wa Taliban kuanza kuwashambulia kwa kulipiza kisasi, wanajeshi wa Marekani na Afghanistan, na kuvianzisha tena vita hivyo.

Uamuzi huu umekuja wakati ambapo Uturuki imetangaza kuandaa mkutano wa kimataifa wa amani kwa matumaini ya kufikia makubaliano kuhusiana na kuleta amani Afghanistan, taifa ambalo limekumbwa na vita kwa karibu miaka 40. Lakini wanamgambo wa Taliban wamesema hawatohudhuria mkutano huo.

Wabunge wa Marekani wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na uamuzi huo huku kiongozi wa chama cha Republican katika bunge la seneti Mitch McConnell akisema "ni sawa na serikali ya Marekani kukiri kushindwa usoni mwa adui ambaye hajaangamizwa."

Lakini sehemu kubwa ya Wademocrat wameonekana kuunga mkono hatua hiyo huku seneta Tim Kaine akisema wanajeshi hao wanastahili kurudi nyumbani na Marekani ijikite katika usalama wa kitaifa na masuala mengine mengi muhimu.

Post a Comment

0 Comments