SUAMEDIA

Majaliwa: Serikali Imetumia Sh. Bilioni166.17 Kugharimia Elimumsingi

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. bilioni 166.17 kutekeleza mpango wa Elimumsingi Bila Ada pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari nchini.



Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeboresha miundombinu ya shule za msingi 1,372 na sekondari 554 kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kukarabati shule 18 za wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 13, 2021) wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

Akizungumzia kuhusu elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 142,179.  “Shilingi bilioni 464 zitatumika kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ukilinganisha na shilingi bilioni 450 zilizotumika kwa wanafunzi 130,883 mwaka 2019/2020”.

Amesema katika mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kuinua kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa kuimarisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini; kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wakufunzi pamoja na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kuhusu suala la ukuzaji wa ajira na ujuzi, Waziri Mkuu amesema  katika mwaka 2020/2021 Serikali imechukua hatua za makusudi hususan utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, sambamba na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania.

“Hadi kufikia Februari, 2021 ajira 594,998 zimezalishwa katika sekta mbalimbali. Kati ya hizo, ajira 314,057 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ajira za Serikali. Vilevile, ajira 280,941 zimezalishwa kupitia sekta binafsi.”

Amesema kupitia Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 18,956 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kati ya hao, vijana 5,538 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi ambapo wanufaika 77 ni watu wenye ulemavu.

Pia, Waziri Mkuu amesema vijana 10,178 wamepewa mafunzo ya kurasimishiwa ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi wa mafunzo ambapo 28 kati yao ni watu wenye ulemavu. “Vilevile, vijana 3,240 wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu kazini (Internship) katika taasisi binafsi na za umma ambapo kati yao wahitimu 92 ni watu wenye ulemavu.”

Amesema katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala ya ukuzaji ajira na kazi za staha katika Sera, Mikakati na Mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahiki pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2020/2021, Serikali imekamilisha tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 inayoonesha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho ikiwemo ukuaji wa uwiano wa uwekezaji kwa Pato la Taifa kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019.

Amesema tathmini hiyo imeainisha changamoto mbalimbali za kisera, kisheria na kiutendaji. “Kutokana na tathmini hiyo, Serikali inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.”

“Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kuvutia wawekezaji. Katika mwaka 2020/2021, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 100, inayotarajiwa kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 536.04 na kutoa ajira 9,085. Sekta ya Viwanda imeongoza kwa kuwa na idadi ya miradi 64 sawa na asilimia 64 na mtaji wa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 370.41.”

Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2021/2022, Serikali itaimarisha uhamasishaji wa fursa za uwekezaji na kuboresha mfumo wa upatikanaji wa taarifa za uwekezaji kwa kufanya tafiti na kuandaa Kanzidata ya Uwekezaji ili kuwa na takwimu sahihi za uwekezaji wa ndani na nje ikiwa ni pamoja na idadi ya miradi ya uwekezaji, thamani na ajira zinazozalishwa kutokana na uwekezaji huo.

 (Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Post a Comment

0 Comments