SUAMEDIA

Waziri Mkuu aagiza Wataalam wa Michezo waendelezwe

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ziandae mkakati wa kuendeleza wataalam wa michezo, sanaa na burudani nchini.


“Miongoni mwa changamoto zinazoikumba sekta ya  michezo, sanaa na burudani ni eneo la kiufundi na mbinu. Hili linadhihirishwa na uwepo wa walimu wengi wa kigeni hususan kutoka baadhi ya nchi jirani kwenye mchezo wa soka”.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Aprili 13, 2021) wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa Fedha 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema licha ya kuendelea kukua kwa sekta ya sanaa, michezo na burudani nchini bado mchango wake katika uchumi ni mdogo. “Kwa mfano, tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2019 sekta ya sanaa na burudani ilichangia asilimia 0.3 kwenye pato la Taifa”.

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema sekta hiyo inapata hamasa kubwa, inaajiri vijana wengi na kwa sasa na imekuwa miongoni mwa sekta zinazotumika kulitangaza Taifa nje na wakati mwingine kuvutia utalii.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh.116,784,244,000.00 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa matumizi ya mwaka 2021/2022. Amesema kati ya fedha hizo, sh. 93,303,370,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 23,480,874,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

“Mheshimiwa Spika, vilevile naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 128,873,377,000.00 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 121,875,906,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na shilingi 6,997,471,000.00 ni kwa ajili ya maendeleo.”

 (Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Post a Comment

0 Comments