SUAMEDIA

Wanawake watakiwa kujitathimini walikotoka walipo sasa na wanakoelekea

 Na.Vedasto George.


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa amewataka Wanawake mkoani humo kutumia  kaulimbiu ya siku ya  Wanawake Dunia inayosema Wanawake katika Uongozi ni Chachu ya kufikia Dunia yenye Usawa  kwa kujitathimini walikotoka walipo sasa na wanakoelekea.



Rai hiyo ameitoa  katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika Machi 8 kila mwaka na kusema wanawake wanatakiwa kutumia muda na fursa zilizopo mkoani Morogoro ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Sasa niwaombe wakina mama  na hasa wakina mama vijana kugawanya muda wako vizuri usitumie muda mwingi kulaumu na kujilaumu  tumia muda wao mwingi kujipanga katika maisha  fursa ya kukopa ipo Maafisa Maendeleo wa Kata,maafisa Maendeleo wa Manisapaa tuwatumie  tuwe wag’ang’anizi wa kiuchumi ukianza kukata tamaa mwenyewe hakuna atakayekusaidia Alisema Msulwa.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Morogoro amewataka vijana wa kike kushikamana na kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mikopo ya asilimia kumi isiyo na riba inayotolewa katika Halmashauri.

Tuitumie hiyo hela vizuri kuna wengine wakishapata fedha hiyo ndio wanaenda kumtoa mwali  ukiifanya fedha ya mkopo kuwa ya sikukuu utaishi bila amani kumbuka mkopo huo lazima urudishwe lakini niwaase ukishachukua mkopo huo fanya yanayotakiwa pia zingatia kurudisha ili na wengine waweze kupata”. Alisema Msulwa.

Akisoma Risala kwa niaba ya wanawake wa mkoa wa Morogoro Bi. Heriety Mkanga amesema changamoto kubwa zinazo wakabili wanawake katika mkoa wa Morogoro ni pamoja na kukosa uelewa juu ya upatikanaji wa mitaji mikubwa ambayo itawawezesha wanawake kuweza kujikimu katika biashara na kuendesha familia zao.

Amebainisha kuwa mikopo inayotolewa na Serikali kwa vikundi vya wajasiriamali hususani wakinamama ni midogo ambayo haiwezi kukamamilisha  malengo ya wanawake katika kujikwamua kiuchumi na kuweza kutekeleza adhma ya Serikali ya kufikia uchumi wa viwanda.

Tunaomba kiasi cha mkopo kiongezwe ili tuweze kujikita katika shughuli kubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogovidogo,vya kati na hata vikubwa, changamoto nyingine mgeni rasimi ni ukosefu wa masoko wanawake tumekuwa tukijishughulisha na kilimo, usindikaji,ufugaji, lakini bado bidhaa zetu hazina uhakika wa masoko”.Alisema  Bi. Mkanga

Kwaupande wake Dkt Charles Lyimo Mwenyekiti wa Masuala ya Kijinsia katika Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA amesema SUA kwa kutambua usawa wa kijinsia Chuo kimeunda sera ambayo tayari imepitishwa na Baraza la Chuo na tayari imeanza utekelezaji ili iweze kusimamia masuala ya usawa  chuoni hapo

“Sera ya usawa ya Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA ilifanyiwa marekebisho mwaka 2012 na kuboreshwa zaidi ikiwa ni kutokana na mahitaji kadiri inavyotakikana". Alisema Dkt Charles Lyimo.   

 

Naye Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA Bi. Gaudensia Mchotika amewataka wafanyakazi pamoja na wanafunzi katika Chuo hicho kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za kuwepo kwa viashiria vya unyanyasaji wa kijinsia ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Katika ofisi zetu  ukiingia ofisi ambazo unaona kabisa kuna viashiria vya kutongozwa  usithubutu kumsogelea awe mwanamke au mwanaume kwa sababu unavyomsogelea akikugusa tu watu ni wajanja anaweza kukugusa sehemu ambazo sio  na ikawa kwako rahisi  kukupata" alisema Bi. Mchotika Mwenyekiti wa RAAWU SUA MOROGORO.

 

Post a Comment

0 Comments