NA: HADIJA ZAHORO
Wanawake watakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kutimiza majukumu yao ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unapatikana kwa wao kushirikiana katika kuleta haki sawa na hatimaye kuwa na maendeleo endelevu kulisukuma taifa kufikia dunia yenye usawa.
Hayo yamesemwa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Yasinta Muzanila wakati wa kufungua Semina kwa wanajumuiya wa SUA katika maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani, ambapo amewataka wanawake hao kuwa mabalozi kwa watakayojifunza kupitia semina ambayo imeandaliwa na chama cha wafanyakazi RAAWU, THTU, wakishirikiana na dawati la jinsia SUA
Akizungumzia kuhusu Uongozi Prof. Muzanila amesema kuwa ni vema wanawake wakapewa haki sawa katika masuala ya Uongozi kwani kwa kufanya hivyo wanawake hao watakuwa chachu ya maendeleo nchini
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Mkoani Morogoro Dkt. Lulu Ganda akiwasilisha mada juu ya wanawake na uongozi amewashauri wanawake kuwa na uchu wa kutamani kutafuta sifa za uongozi ili kutatua suala la ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kuwa wanawake wasisite kujitokeza na kukemea ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake pia elimu juu ya haki sawa katika jinsia izidi kutolewa katika jamii na kuwataka watumishi wa vyuo nchini kutoa elimu kwa wanafunzi vyuoni.
Akiwasilisha mada juu ya Athari za Unyanyasaji wa kingono kwa ufanisi na tija ya Taasisi za Elimu ya Juu, Mshauri Mwandamizi wa Jinsia na Afya ya Uzazi, Dkt. Katanta Simwanza amesema ni vyema jamii kuelewa athari za unyanyasaji wa kingono ambazo zinashusha hari ya kufanya kazi,ufanisi wa kazi,kukosa haki za msingi na kuambukizana magonjwa.
Ameeleza Athari nyingine zitokanazo na unyanyasaji wa kingono ni pamoja na,kuwepo na visa au ukandamizaji makazini, ubunifu na ugunduzi kutoweka na kushusha uwezo wa watu katika taaluma.
Siku ya wanawake duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8 ambapo kwa mwaka huu Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo ‘‘Wanawake katika Uongozi:Chachu Kufikia Dunia yenye Usawa”.
0 Comments