SUAMEDIA

Vyuo Vikuu nchini hakikisheni mnatafuta suluhisho la kuchakata mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani - Mwenyekiti PAC Mhe. Kaboyoka

 

Na Gerald Lwomile

Morogoro

Vyuo Vikuu nchini kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) vimeshauriwa kuhakikisha vinatafuta suluhisho la kuchakata mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani na kuondokana na dhamira ya wakoloni ya kutaka kuhakikisha nchi za Afrika zinasafirisha malighafi tu katika nchi zao

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka akisikiliza maelezo kutoka kwa Makamu wa Mkuu  wa SUA Prof. Raphael Chibunda 

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo katika chuo cha SUA ambayo imelenga kuona maendeleo ya ujenzi wa Maabara Mtambuka inayojengwa chuoni hapo

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka akifafanua jambo wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo

Mhe. Kaboyoka ameongeza kuwa zamani wakoloni walitumia njia ya udanganyifu kuhakikisha Waafrika wanashindwa kuongeza thamani ya mazao kwa kuchakata bidhaa na kusababisha kuendelea kuwa soko la bidhaa zao huku malighafi yote inayozalisha bidhaa hizo ikitokea Afrika

Amesema kuwa SUA pia ina wajibu wa kuhakikisha mazao yanayozalishwa na wakulima yanapata soko na mengine kuongezewa thamani hapa hapa nchini jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi wa nchi

“Mtu anatumia gharama katika uzalishaji, ananunua pembejeo, anachukua mkopo na anatumia gharama kubwa katika uzalishaji halafu mwisho anaambiwa hakuna soko, inasikitisha sana” amesema Kaboyoka

Naye Makamu Mwenyekiti wa PAC Mhe. Japhet Hasunga amesema anashangazwa na namna Maabara za hapa nchini zinavyoshindwa kubaini mbolea na madawa feki yanayoingizwa na kuleta hasara kubwa kwa wakulima na wafugaji


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka katikati aliyevaa nguo nyekundi akiwa katika picha ya pamoja baada ya kukagua jengo la Maabara Mtaambuka SUA ( Picha zote na Gerald Lwomile)

Amesema ni muhimu sasa kama nchi kuhakikisha kunakuwa na Maabara ambazo zinaweza kupima ubora wa mbolea na madawa ili kuhakikisha mkulima wa Tanzania anapata pembejeo hizo na zinamsaidia

Akijibu baadhi ya hoja za Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema SUA tayari imefanya jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu masomo chuoni hapo wanaweza kuongeza thamani ya mazao kwa kuanzisha viwanda mbalimbali

Amevitaja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni pamoja na vijana walionzisha viwanda vya kuongeza thamani katika maziwa na mazao ya nyuki.

Aidha amesema kuwa Maabara ya Udongo iliyoko chuoni hapo ina uwezo wa kupima udongo pamoja na kujua ubora wa mbolea  na kwamba imeendelea kufanya vizuri baada ya serikali kukiwezesha chuo kununua mitambo ya kisasa ya kuiwezesha maabara hiyo kufanya kazi kwa ufanisi.


                                  Muonekano wa Maabara Mtambuka SUA

Kamati hiyo ya PAC imefanya ziara hiyo ya siku moja na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Maabara Mtambuka  iliyo katika hatua za mwisho za ujenzi ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 11, ambapo Serikali Kuu imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 9 na bilioni 2.6 zikiwa ni mapato ya ndani ya chuo


Post a Comment

0 Comments