Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwenzake wa Botswana Eric Mokgweetsi Masisi wamekubali kuendelea kuzungumza kutafuta suluhisho kuhusu suala la wadhifa wa Katibu Mtendaji wa SADC.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwenzake wa Botswana Eric Mokgweetsi Masisi wamekubali kuendelea kuzungumza kutafuta suluhisho kuhusu suala la wadhifa wa Katibu Mtendaji wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika-SADC.
Akiwa ziarani mjini Kinshasa jana Jumatatu, Rais Masisi alizungumza ana kwa ana na Tshisekedi. Viongozi hao wawili wamejadili maswala mengine kadhaa yakiwemo na kupambana na janga la Covid-19.
Botswana ilikuwa ya kwanza kuwasilisha ombi la kugombea nafasi ya Katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC. Nafasi hiyo itakuwa wazi Agosti ijayo, lakini hii imekutana na changamoto baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia kutangaza pendekezo lake.
Marais wa nchi hizo waweka bayana kuwa wataendelea kujadiliana
Bwana Elias Magosi wa Botswana na Faustin Luanga Mukela wa Kongo ndio wagombea wawili. Nchi hizo mbili tu ndizo zinakubaliwa kuwasilisha mgombea wa nafasi hiyo ya Katibu Mtendaji wakati huu.
Marais wawili wataendelea kujadiliana, kama alivyoeleza Éric Masisi wa Botswana. "Kongo ina mgombea anayestahili ambaye wamempendekeza kama Katibu Mtendaji atakayechaguliwa kwenye mkutano ujao. Botswana vile vile, ina mgombea muhimu ambaye tumemtambulisha rais tukiomba atuunge mkono. Tumekubali kuendelea na majadiliano ili tupate suluhisho kwa amani. Tutaendelea kuwasiliana." amesema Masisi.
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi kwa sasa anaongoza Umoja wa Afrika, wakati rais wa Botswana Éric Masisi ndiye mwenyekiti wa tume ya jumuiya ya SADC inayohusika na siasa, ulinzi pia usalama.
Na ndio maana viongozi hawa wawili wameyagusia pia maswala mengine kadhaa. Jambo ambalo limemridhisha Rais Tshisekedi kama alivyoeleza "Kutafanyika mambo makuu baina ya nchi zetu mbili kwa masilahi ya raia wetu na hii itanifurahisha. Inaambatana na yale tuliyojadiliana wakati tulipokutana Novemba iliyopita. Rais Masisi alinialika nchini Botswana ili kujaribu kuzileta pamoja nchi zetu mbili katika sekta mbalimbali. Nimefurahishwa sana."
Kinshasa na Gaborone wanaishi katika uhusiano mzuri na ziara hii ya kikazi ya Rais Masisi aliyokuwa nayo hapa, imekuja kuimarisha zaidi uhusiano uliopo.
0 Comments