Na Farida Mkongwe, Morogoro
Wafugaji
wa kuku wameshauriwa kuhakikisha wananunua vifaranga kutoka kwenye mashamba
ambayo yanatoa chanjo za awali ili kuepusha vifo vya vifaranga ambavyo
vinasababisha hasara kwa mfugaji.
Ushauri
huo umetolewa na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambaye
pia ni Daktari wa Mifugo Amina Ramadhani Issae wakati akizungumza na SUAMEDIA
kwenye moja ya banda alilotembelea lililopo eneo la Nane Nane mjini Morogoro
kwa ajili ya kutoa chanjo ya ndui ya kuku.
Daktari
Issae akiwa ameambatana na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya kwanza ya
Udaktari wa Mifugo kutoka Ndaki ya Tiba za Wanyama na Sayansi za Afya amesema
chanjo ni jambo la msingi sana katika kuhakikisha kuku wanakuwa na afya njema.
“Mfugaji ni lazima ahakikishe anaijua historia ya shamba analonunua vifaranga kwa sababu kuna mashamba mengine yanauza vifaranga bila kuwapa chanjo za awali ikiwemo mareks, na pia ahakikishe shamba hilo halina historia ya magonjwa”, alisema Daktari huyo.
Aidha
Mtafiti huyo kutoka SUA amewataka wafugaji kuzingatia mahitaji muhimu kwenye
uchanganyaji wa chakula ili kuku waweze kupata virutubisho vyote
vinavyohitajika pamoja na kuzingatia usafi wa banda na kuhakikisha banda
linakuwa na hewa ya kutosha.
Daktari aliyeshika kuku akiwaelekeza wanafunzi namna ya kutoa chanjo ya ndui
Kwa
upande wao baadhi ya wanafunzi akiwemo Boniventure Bundara na Jumanne Ibrahim
wamewashauri wafugaji kuwa na vyumba vya kutosha kwenye mabanda yao na
kuwagawanya kuku kulingana na umri wao ili kuweza kuwapa chakula kwa kuzingatia
hatua mbalimbali za ukuaji pamoja
na kuzuia magonjwa ya kuambukiza.
0 Comments