SUAMEDIA

Ununuzi wa Mazao kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani na Mikataba umewainua wakulima



Na Gerald Lwomile

Simiyu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa amesema  katika kipindi cha mwaka 2018/2019 mazao yenye thamani ya sh. trilioni 2.9 yameuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani au kupitia Mkataba jambo ambalo limewasaidia wakulima kupata bei nzuri na wanunuzi kupata mazao bora yenye uhakika


Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki akisoma hotuba ya Waziri Mkuu

Hayo yamesemwa leo Agosti 3, 2020 katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki ambaye amemuwakilisha Waziri Mkuu katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa Nyakibindi, Bariadi Mkoani Simiyu

Mhe. Majaliwa amesema uuzwaji wa mazao kupitia vyama vya ushirikika uzingatia mambo mbalimbali kama uhakika wa vipimo vya mazao, madaraja na ubora wa mazao lakini pia unaisaidia serikali kupata takwimu za uzalishaji na kutoa bei shindani

“Na kwa mfano wa hili ukiangalia kwa bei ya zao la kakao imeweza kuimarika na kukua kutoka shilingi 3200 kwa kilo hadi kufikia shilingi 5011 kwa kilo na haya ni matunda na manufaa mazuri ya mfumo wa stakabadhi ghalani tangu mfumo huu uanze kuimarika”,amesema Mh. Majaliwa.


Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki akisikiliza maelezo kutoka kwenye mabanda ya waoneshaji

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amevitaka vyama vya Ushirika nchini kuhakikisha vinawaongezea ujuzi watumishi katika vyama hivyo ili kuongeza ufanisi, tija lakini pia kutasababisha kuwepo kwa uhakika wa kudumu kwa vyama hivyo

Aidha Waziri Mkuu amesema serikali haitasita kuwachulia hatua wabadhirifu katika vyama vya usharika kama ilivyofanya hivi karibu kwa kuhakikisha inarejesha mali zote za ushirika zilizokuwa zimeporwa na viongozi wasio waaminifu


Post a Comment

0 Comments