SUAMEDIA

SUA yaendelea na utafiti wa kubaini dawa za kudhibiti Mende na Kunguni

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kinaendelea na utafiti wa
kubaini dawa za kuwadhibiti mende na kunguni ambao wamekuwa ni
visumbufu sugu kwa binadamu.




Hayo yamebainishwa na Mtafiti ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi
wa Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu SUA Dkt. Abdul
Katakweba wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye mabanda ya
chuo hicho yaliyopo kwenye maonesho ya nanenane Kanda ya
Mashariki mkoani Morogoro.
Dkt. Katakweba amesema utafiti huo una lengo la kubaini aina ya
kunguni na aina ya dawa zinazofaa kuwadhibiti kunguni hao huku
kwa upande wa mende akisema kuwa wamejikita katika uzalishaji wa
mende wenye faida ambao ni chakula cha mifugo sanjari na kujua
dawa ya kuwadhibiti mende ambao hawana faida.
Aidha Dkt. Katakweba amezungumzia teknolojia ya mifuko ya
kuhifadhia mazao na kusema kuwa teknolojia hiyo imeshawafikia
wakulima na imeshaanza kuonesha mafanikio.
“Zamani ilikuwa wakulima wakihifadhi mazao yao yalikuwa yakianza
kubungua baada ya miezi mitatu hadi sita lakini kwa sasa kwa
kutumia hiyo mifuko maalum ya kuhifadhia mazao wakulima
wanaweza kukaa kuanzia miaka mitatu hadi saba bila mazao yao
kuharibika”, alisema Dkt. Katakweba.

Mtafiti huyo ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro kufika
kwenye banda la SUA ili waweze kupata elimu ya jumla ya jinsi ya
kuwadhibiti wadudu waharibifu wa mazao, kupata huduma hiyo ya
mifuko pamoja na elimu ambayo italeta tija kwa wakulima na
wafugaji.

Post a Comment

0 Comments