SUAMEDIA

Ulaji wa matunda ambayo yameliwa na popo yanaweza kuleta madhara kiafya - Dkt. Sijali

Na:Farida Mkongwe
Watanzania hasa waishio vijijini wametakiwa kuacha tabia ya ulaji wa matunda yaliyoliwa na wanyamapori ili kuepukana na magonjwa yanayoweza kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.


Wito huo umetolewa na Mtafiti kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na
Sayansi za Afya iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Dkt.
Sijali Zikankuba wakati akizungumza na SUAMEDIA katika
Maonesho ya Nanenane ya Wakulima yanayofanyika mkoani
Morogoro.
Dkt. Zikankuba amesema ulaji wa matunda mfano maembe ambayo
yameliwa na popo yanaweza kuleta madhara makubwa kiafya kwa
binadamu kwa sababu utafiti umebaini kuwa wanyama jamii ya
popo, nyani na panya wana virusi vinavyoweza kusababisha
magonjwa kwa binadamu.
“Kihistoria magonjwa makubwa kama ebola na hata huu ugonjwa
unaoisumbua dunia kwa sasa yaani corona iliyoanzia nchini China
unatokana na wanyama wa porini, ni muhimu kujikinga na mazingira
hatarishi ili tusipate haya magonjwa”, alisema Dkt. Zikankuba.
Amezitaja baadhi ya tabia nyingine hatarishi kuwa ni  kutumia
vyakula vilivyotumiwa na kubakizwa na wanyama kama panya mfano
mahindi pamoja na kushirikiana vyanzo vya maji na wanyama mfano
kisima, chemichemi au mto. 

  

Post a Comment

0 Comments