Mgombea wa urais wa chama cha Democratic Joe Biden na mgombea mwenzake Kamala Harris wamemshambulia rais Donald Trump wakisema anapenda "kulalamika" na kuongeza kuwa ni kiongozi asiyefaa aliyeiacha Marekani katika "hali mbaya".
Wawili hao walifanya kampeini ya kwanza pamoja siku moja baada ya Bwana Biden kumzindua Bi. Harris kama mgombea mwenza.
Rais Trump amejibu tamko lao kwa kusema Bi Ms Harris "ameanguka kama jiwe" katika jaribio lake la kuwania urais.
Biden atamenyana na Trump, wa Republican, katika kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mwezi Novemba.
Biden amesema nini?
Hafla hiyo iliyoandaliwa usiku wa Jumatano mjini Wilmington, Delaware, haikua wazi kwa umma, baada ya Bw. Biden, 77, kuzingatia hofu ya maambukizo ya virusi vya corona. Wagombea wote walipanda jukwaani wakiwa wamevalia barakoa na kuzungumza na kundi la wanahabari waliokua pia wamevaa barakoa na kuhakikisha hawakaribiani.
Karibu watu 75 walihudhuria hafla hiyo kukutana na wagombea hao wawili, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, japo baadhi yao walikua wakimkosoa Bw. Biden.
Akizungumza katika jukwaa la shule ya upili ya Alexis I DuPont, Bwana Biden alimtaja Bi Harris, Seneta wa California, kama mwanamke wa kwanza mweusi kushikilia wadhifa wa kuwa mgombea mwenza wa urais katika chama kikubwa nchini Marekani.
Bw. Biden alisema: "Uamuzi tutakaofanya mwezi Novemba utaamua hatima ya baadae ya Marekani kwa muda mrefu sana."
Aliendelea kusema : "Donald Trump ameanza mashambulizi yake, kwa kumuita Kamala, nikimnukuu, ni mjeuri, akilalamika jinsi kiongozi huyo unavyomuonea mgombea mwenzake.
"Halo halinishangazi kwa sababu kulalamika ni hulka ya Donald Trump, ameweza kufanya hivyo kuliko rais mwingine yeyote katika historia ya Marekani.
"Kuna mtu yeyote anabisha kwamba rais Trump ana matatizo na wanawake wanaojiamini katika kila fani?"
Pia alikosoa jinsi Bw. Trumpa alivyoshughulikia janga la corona,mabadiliko ya tabia nchi,suala la ukosefu wa ajira na "siasa zake zinazoegemea ubaguzi wa rangi na kuleta mgawanyiko ".
Harris alisema nini?
Bi Harris alipanda jukwani na kusema: "Niko tayari kufanya kazi."
Kiongozi huyo wa zamani wa mashitaka mwenye umri wa miaka 55 amewaambia waandishi wa habari: "Huu ni wakati utakaoangazia hali halisi ya changamoto za Marekani. Kila kitu tunachojali, uchumi wetu, afya yetu, watoto wetu, nchi yetu na vyote vilivyomo ndani."
Bi Harris - binti wa wahamiaji kutoka India na Jamaica - aliendelea kusema: "Marekani inalilia uongozi, lakini tuna rais anayejali malahi yake binafsi kuliko maslahi ya watu waliomchagua."
Aliendelea kusema: "Yeye [Bw.Trump] amerithi utawala ulikua na uchumi ulioimarika katika historia ya Marekani chini ya utawala wa Barack Obama na Joe Biden.
"Badala ya kuendeleza nchi, kutoka mahali alipoachiwa, alididimiza kila kitu."
Bi Harris alisema: "Haya ndio mambo yatakayokukuta unapomchagua mtu ambaye hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake - nchi yetu itakosa maana na kupoteza hadhi yake kote duniani."
CHANZO BBC SWAHILI
0 Comments