SUAMEDIA

TAWFA yatoa wito kwa Taasisi za Fedha na Halmashauri ziwatazame wavuvi


Na Ahmad Mmow, Lindi. 
Taasisi za fedha na halmashauri nchini zimeombwa kutupia jicho sekta ya uvuvi kuhusu mikopo. 

Wito huo ulitolewa jana na katibu wa Umoja wa Wavuvi Wanawake Tanzania(Tanzania Woman Fisheries Asociation/TAWFA), Hadija Malibiche  katika viwanja vya Ngongo, manispaa ya Lindi yanapofanyika maonesho ya wakulima( Nanenane) kanda ya Kusini. 


Malibiche alisema licha ya kushikwa mkono na Wizara ya Mifugo na Uvuvi bado kuna changamoto ya wavuvi kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na halmashauri kupitia asilimia kumi zinazotokana na vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali. 

Alisema wavuvi wanachangamoto ya mitaji. Hatahivyo taasisi za fedha zimekuwa na masharti magumu ya kuvipa mikopo. Masharti na vigezo ambavyo ni vigumu kutekelezeka. 

 '' Sisi tulitaka tukope shilingi milioni ishirini, lakini benki ilitutaka tuwe na dhamana ya shilingi milioni tano ambazo hatuna. Tunashindwa kujua kwani hawatuamini, umoja wetu nidhamana tosha. Hata halmashauri zinasuasua kuwakopesha wavuvi nikama hatuaminiki,'' alisema Malibiche. 

Kufuatia hali hiyo, katibu huyo alitoa wito kwa taasisi za  fedha nchini ziwape masharti na vigezo rafiki ili sekta ya uvuvi ishiriki kikamilifu ujenzi wa uchumi na maendeleo ya nchi. 

 Kuhusu halmashauri Malibiche ameziomba ziwakopeshe wavuvi kama wajasiriamali wengine. Kwani soko la mazao ya uvuvi ni kubwa lisilo na shaka. Kwahiyo wanauwezo wakurejesha mikopo kwawakati. 

'' Tunaposema wavuvi nipamoja na wanaochakata samaki na wachuuzi hata wanaotembeza mitaani kwenye masinia. Wote hao wanahitaji kusaidiwa ili wanyanyuke,'' alisisitiza. 

 Kuhusu ushirikiano na wizara alisema tangu TAWFA iasisiwe na kuanza kufanyakazi imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa toka wizara ya mifugo na uvuvi. Kwani ni wizara hiyo iliyowahamasisha waanzishe umoja huo. 

Lakini ya kukiri kupata ushirikiano,   alishauri sheria ya uvuvi iwatambue kikamilifu wanawake, iwapatie mafunzo ya fedha, masoko ,ufungashaji bidhaa na masuala yanayohusu jinsia. Huku akitoa wito kwa wanawake waachane na dhana kwamba sekta ya uvuvi ipo kwa ajili ya wanaume peke yao. 

 Kwaupande wake ofisa uvuvi mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Melkizedeck Koddy alisema wizara kupitia dawati la sekta binafsi itaendelea kuwaunganisha wavuvi na taasisi za fedha ili wapate mikopo. 

 Alisema kwakutambua umuhimu wa wavuvi katika kuchangia ujenzi wa uchumi wao na wataifa. Kwahiyo itaendelea  kuwasaidia kuandaa maandiko ambayo yatarahisisha upatikanaji mikopo. 


Post a Comment

0 Comments