Habari na Mwandishi wetu
Ili kuchangia
katika utekelezaji wa Awamu ya Tatu (iliyoanza mwaka 2017 na itayomalizika
mwaka 2022) ya Mkakati wa Taifa wa Kupambana
na Rushwa, Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA), kupitia Kamati ya Kuthibiti Uadilifu ya SUA (KKU-SUA),
kimeendelea kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake.
Mwenyekiti wa KKU Prof. Mahonge wa pili kulia akiwa na wajumbe wa KKU na wafanyakazi walioshiriki mafunzo katika
Kampasi ya Olmotonyi Arusha
Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 18 na 19 ya mwezi Agosti mwaka 2020 katika Kampasi za SUA zilizo nje ya Mkoa wa Morogoro, yaani Kampasi ya Olmotonyi mkoani Arusha, na Kampasi ya Mazumbai mkoani Tanga.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Christopher Mahonge amesema SUA imeazimia kwa dhati kuhakikisha inathibiti uadilifu na kudhibiti rushwa katika maeneo yake ya kazi.
Amesema hatua muhimu ya kwanza katika kulifikia lengo hilo, ni
kuhakikisha wafanyakazi, hasa waajiriwa wapya, wanaelimishwa kuhusu kanuni na
miongozo ya uadilifu kwa watumishi wa umma. Pamoja na mambo mengine, aliwaasa
wafanyakazi kujiepusha na
majungu katika maeneo ya kazi, na kushirikiana na kamati kwa kuwasilisha
taarifa zozote za malalamiko zinazohusu chuo kutoka vyanzo mbalimbali kama vile
mitandao ya kijamii, na vyombo vya habari.
Wajumbe wa KKU na wafanyakazi walioshiriki mafunzo katika Kampasi ya Mazumbai Lushoto
Naye Mjumbe wa kamati hiyo Dkt. Abdul Katakweba,
akizungumza na wafanyakazi katika kampasi hizo kupitia wasilisho lake, amesema majukumu
ya KKU ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mpango kazi wa mapambano dhidi ya
rushwa katika taasisi. Aliongeza kuwa, majukumu mengine ya kamati ni kuandaa
taarifa za utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini za robo mwaka na mwaka na
kuwasilisha kwa Kamati ya Uongozi ya Usimamizi, na kupokea, kuchambua na
kushughulikia malalamiko toka ndani na nje ya Taasisi yanayotokana na ukiukwaji
wa maadili.
Mawasilisho kutoka
kwa Prof. Mahonge na Dkt. Katakweba yalitanguliwa na na maelezo ya maana za
maneno matatu yaliyotumika kwenye mawasilisho, yaani Uadilifu, Rushwa na Uwajibikaji.
Bibi Lightness Mabula, ambaye ni mjumbe wa kamati, alitoa tafsiri ya neno uadilifu; Bw.
Nicholaus Mwamtobe, ambaye pia ni Mjumbe wa kamati, akaelezea
maana ya neno rushwa, wakati Prof. Mahonge alielezea maana ya neno uwajibikaji.
Baada ya mawasilisho, wafanyakazi wa
Kampasi za Mazumbai na Olmotonyi walipata muda wa kujadili na kuuliza maswali
na kutoa maoni yanayohusiana na masuala ya uadilifu na kupata ufafanuzi zaidi
kutoka kwa wajumbe wa KKU-SUA.
Hatua inayofuata baada ya mafunzo hayo ni
kuwapata wawakilishi wawili kutoka katika kila kampasi, mwanamke na mwanaume,
ambao watakusanya malalamiko yahusuyo ukiukwaji wa maadili kutoka kwa
wafanyakazi wanaowawakilisha na kuyawasilisha kwa KKU-SUA kwa ajili ya
kufanyiwa kazi na kutafutiwa ufumbuzi.
0 Comments