Na: Calvin Gwabara, Katavi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe
ameridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo SUA kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi na kuanza rasmi kwa Kampasi ya
Mizengo Pinda Mkoani Katavi.
Prof. Mdoe ameyasema hayo wakati alipotembelea kampasi hiyo mpya ya SUA
iliyopewa jina la Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda alipokwenda kujionea
maandalizi na mazingira ya kampasi hiyo ambayo inatarajia kupokea wanafunzi
tarehe 23/11/2020.
Naibu katibu Mkuu huyo amesema uanzishwaji wa Kampasi hiyo unasaidia jitihada
za Serikali kupitia Wizara yake kwenye kuongeza nafasi nyingi zaidi za
wanafunzi wenye sifa na wanaotaka kusoma elimu ya juu hasa baada ya maboresho
makubwa ya elimu yanayofanywa na Serikali nchi nzima kwenye elimu ya Msingi na Sekondari.
“ Kwanza niwapongeze sana SUA na uongozi mzima kwa kazi kubwa ambayo
mmeshaifanya ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kampasi hii, na sisi kama
Wizara tunawaahidi kuwasaidia ujenzi wa bweni kubwa haraka ili mwaka ujao wa
masomo iwe imekamilika na itumike kuwezesha wanafunzi kuishi vizuri maana najua
watakuwa wengi” Alisema Prof. Mdoe.
Pia ametumia nafasi hiyo kuwashauri SUA kuanzisha kozi fupifupi zitakazoweza
kusaidia kuleta ujuzi kwa wananchi wa eneo hilo na mkoa kwa ujumla ambazo
hazihitaji mtu kuwa na sifa bali kutoa ujuzi kulingana na mahitaji ya wananchi
hasa wale ambao hawajafika kidato cha nne.
Naibu katibu Mkuu huyo awepongeza uzalendo Mkubwa aliouonyesha Waziri Mkuu
mstaafu Mhe. Mizengo Pinda kwa kuyatoa majengo hayo na ardhi kama shamba kwa ajili
ya kuanzisha kampasi hiyo na kuitaka jamii kuiga mfano huo.
Akitoa taarifa fupi ya kampasi hiyo ya Mizengo Pinda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda ameishukuru Serikali kwa
jitihada kubwa ambazo inazifanya katika kuboresha mazingira ya kufundishia kuanzia Shule za Msingi
hadi Vyuo Vikuu na hivyo kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupata elimu.
Prof. Chibunda amesema mara baada ya kukabidhiwa majengo hayo na Waziri Mkuu
huyo Mstaafu Mhe. Pinda waliofanya tathimini na kutenga kiasi cha shilingi
milioni 200 kwa ajili ya ukarabati lakini hadi kufikia hapa tayari wameshatumia
kiasi cha shilingi milioni 810 na bado kazi inaendelea ili kuwezesha wanafunzi
watakapoingia mazingira yote yawe tayari.
Ameongeza kuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu alipata nafasi ya
kunitembelea Kampasi hiyo yeye mwenyewe na anashukuru kuwa sasa wamepata
ithibati ya kuanza kupokea wanafunzi kwa Mwaka huu kwa Kozi tatu maalumu
kulingana na mahitaji ya Mkoa wa Katavi na mikoa mingine jirani.
“ Maono yetu kama Chuo ni kuona ukanda huu unakuwa na Chuo kikubwa na hivyo
kuchochea elimu na ujuzi kwa wananchi badala ya wahitimu kwenda mbali kama
Morogoro na Dar es Salama kusoma Vyuo Vikuu, hapa ni mahali sahihi sana kwa
kutolea elimu pengine tofauti na maeneo mengine hivyo ni matumaini yetu kuwa
vijana wa maeneo haya watakuwa wengi kuliko mikoa mengine” Alisema Prof.
Chibunda.
Akizungumzia Kozi zitakazoanza kutolewa katika Kampasi hiyo Mkuu wa
Kampasi hiyo Prof. George Mwamengele amesema wataanza na kozi tatu ambapo moja
ni Astashahada ya Uongozaji Watalii na Uwindaji Salama, kozi ya pili ni
Stashahada ya Kilimo na kozi ya tatu ni Shahada ya Nyuki na Mazao yatokanayo na
Nyuki.
Prof. Mwamengele amesema maandalizi kwa kiasi kikubwa yamekamilika kwa maana ya
miundombinu kama vile madarasa, mabweni, mifumo ya mtandao lakini pia Chuo
kimeajiri walimu wapya wa kutosha na wengine wakongwe wamehamishwa kutoka Kampasi
ya Morogoro na kuletwa Mizengo Pinda
Dirisha la maombi kwa wanafunzi wa kozi mbalimbali kwenye Kampasi Kuu na kampasi
hii mpya ya Mizengo Pinda litakuwa wazi kuanzia tarehe 31/08/2020 na Wanafunzi
kwa mujibu wa kalenda ya masomo wanatakiwa kuwasili Chuo kwaajili ya kuanza
masomo tarehe 23/11/2020.
0 Comments