SUAMEDIA

SUA iko tayari kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzalisha mitungi ya kuhifadhia Chanjo


Na Gerald Lwomile, Simiyu


Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimesema kiko tayari kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzalisha kwa wingi mitungi ya kuhifadhia chanjo ili iwasaidie wafugaji katika kuhifadhi chanjo na kuleta ufugaji wenye tija
Prof. Chibunda akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani juu ya mitungi ya kuhifadhia chanjo

Hayo yamesemwa Agosti 7, 2020 Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitaka kujua SUA imeichukuliaje kauli ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi aliyetaka Wizara yake kushirikiana na SUA ili kusambaza ubunifu huo

Prof. Chibunda amesema ubunifu na teknolojia hiyo rahisi utawasaidia wakulima katika maeneo ambayo yana changamoto ya umeme kuhakikisha wataalamu wa mifugo wanahifadhi chanjo hizo ili zibaki salama na kuendelea kuchanja wanyama mbalimbali kama mbwa, ng’ombe, mbuzi na wengineo wengi

“Kauli ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi tumeipokea kwa furaha, na kwa sababu tumeshatoka kwenye hatua ya utafiti sasa hivi mitungi ipo na tumeanza kuitumia kwa hiyo sisi tutashukuru sana hasa wadau wetu wa Wizara ya Mifugo wakija wakashirikiana na chuo chetu tuweze sio tu kuitengeneza lakini pia kuisambaza”, amesema Prof. Chibunda
Mtungi wa kuhifadhi chanjo uliotengenezwa SUA

Akizungumzia hatua zilizofikiwa za kuhakikisha mkulima anapata  taarifa kwa wakati kuhusu mambo mbalimbali ya kilimo, Prof. Chibunda amesema Maktaba ya Taifa ya Kilimo ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na ipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA iko katika hatua za mwisho kukamilisha programu maalum ya kutumia simu za mkononi katika kupata taarifa na vijitabu mbalimbali

“Lakini kwa kutumia wataalam wetu wa ndani ndiyo wametengeza program maalumu ambayo ukiwa na simu janja unaweza kupata machapisho, lakini tufahamu kuwa wakulima wengi bado hawajanunua simu janja ila wataalamu wetu wanazidi kuangalia ni namna gani hata mtu mwenye simu ya kawaida atapata taarifa kupitia simu yake” amesema Prof. Chibunda
Prof. Chibunda kushoto akisikiliza maelezo kutoa kwa Mwokozi Mwanzalila mtafiti msaidizi katika mradi wa HALI 


Post a Comment

0 Comments