SUAMEDIA

Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuhakikisha wanatumia fursa kupeleka sokoni Tafiti na Ubunifu

Na Gerald Lwomile, Simiyu

Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali kupeleka sokoni tafiti na ubunifu mbalimbali unaofanywa na watafiti ili kuhakikisha wanalisaidia taifa na kuleta maendeleo


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Dkt. Amos Nungu akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 7, 2020 katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema kama wafanyabiashara watazichukua tafiti na ubunifu na kuutumia kwa kuzalisha bidhaa na huduma nchi itapiga hatua kwa kasi

Amesema serikali imefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kufadhili tafiti mbalimbali lakini kuna wakati ubunifu katika sekta ya biashara unatakiwa na wanaoweza kufanya hivyo ni wafanyabiashara katika kutengeneza thamani ya bidhaa

“Kwa taasisi za utafiti zenyewe kazi yake kubwa ni kufanya utafiti na wakati mwingine kufundisha na siyo kufanya biashara lakini kama tunataka kuisaidia nchi kusudi wawe na mazao mengi…..., kwa hiyo wafanyabiashara waone kuwa ni fursa kushirikiana ili kupeleka bidhaa sokoni”, amesema Dkt. Nungu

Akizungumzia tafiti mbalimbali ambazo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekuwa ikizifadhili amesema wanaridhishwa na maendeleo ya tafiti hizo zikiwemo za maktaba ya mkulima, utafiti wa panya SUA na utafiti wa michikichi kama zao la kimkakati unaofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania

Amesema wakati Serikali ya awamu ya tano ikiendelea kuhakikisha kunakuwa na nchi ya viwanda, huwezi kuweka mbali kilimo na viwanda kwani viwanda vingi vinategemea malighafi zitokanazo na kilimo na ili watu wafanye kazi ni lazima wawe na afya njema  na ndiyo maana COSTECH kama Tume ya Sayansi na Teknolojia inahakikisha inasaidia katika kutoa ufadhili wa tafiti na ubunifu mbalimbali nchini

Post a Comment

0 Comments