Na Gerald Lwomile
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samiha Suluhu Hassan amesema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na watafiti na
hasa katika kuvumbua mbegu bora zenye kinga dhidi ya magonjwa pamoja na zile
zinazostahimili mabadiliko ya tabia nchi lakini bado tafiti hizo haziendi kwa
wananchi kwa kiwango cha kutosha
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya ufunguzi wa maonesho ya Nanenane (Picha zote na Gerald Lwomile)
Mama Suluhu amesema hayo leo Agosti 1, 2020 wakati
akifungua maonesho ya wakulima Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi Bariadi
Mkoani Simiyu
Amesema kuwa ni muhimu watafiti wakatoa matokeo ya
tafiti zao kwa Maafisa Ugani ambao ndiyo wako karibu zaidi na wananchi ambao
ndiyo hasa walengwa na wazalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi
Akizungumzia kilimo cha umwagiliaji, Makamu wa Rais
amesema kutokana na kuwepo kwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu
kutumia umwagiliaji ambao unampa mkulima uhakika wa mavuno hata kama kuna uhaba
wa mvua lakini pia Serikali itahakikisha mindombinu ya umwagiliaji inaimalishwa
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi
itahakikisha kuwa miundombinu ya umwagiliaji inajengwa na kusimamiwa vizuri……,
nisisitize kuwa tuwaze unyunyiziaji na si umwagiliaji” amesema Mama Samia
Kuhusu sekta ya uvuvi, Makamu wa Rais amelaani vitendo
vya baadhi ya wavuvi wanaovua samaki bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa ili kusimamia utunzaji wa vyanzo vya mazalia ya samaki ambapo sasa
Serikali imeboresha Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
Awali akimkaribisha mgeni rasmi ili kufungua maonesho
hayo Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema ili kuhakikisha kilimo
kinasonga mbele ni muhimu kuwa na usimamizi thabiti wa maafisa ugani ili waende
kushirikiana na wananchi kwa lengo la kutatua changamoto wanazokutana nazo
katika kilimo
“Jambo jingine ni kuwekeza zaidi kwenye utafiti, maana
bila utafiti ni wazi kabisa hatuwezi kuboresha kilimo chetu. Hivyo, lazima
tuwekeze ipasavyo kwenye utafiti wa mambo mbalimbali yanayohusiana na kilimo”
amesema Hasunga
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akitoa taarifa ya kilimo nchini kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua maonesho
Maonesho ya Nanenane kitaifa yanafanyika Mkoani Simiyu
na kauli mbiu ya maonesho hayo ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Chagua Viongozi Bora”
Wakati huo huo banda la maonesho ya kilimo la Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo limekuwa kivutio kwa wadau mbalimbali ambao
wanafika kujionea teknolojia na bunifu mbalimbali zinazozalishwa na tafiti za SUA
Naye Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo SUA, Taaluma Prof. Maulid Mwatawala ambaye amewaongoza waoneshaji wa
SUA mkoani Simiyu amewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kuja kujionea na kushuhudia
matokeo ya tafiti katika nyanja mbalimbali za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
Waoneshaji kutoka SUA wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Taaluma Prof. Maulid Mwatawala wa nane kutoka kushoto
Aliyekuwa Mbunge wa Busega Mhe. Raphael Chegeni aliyevaa Kaunda Suti rangi ya maziwa akisikiliza maelezo kutoka kwa waoneshaji wa SUA aliyevaa kosia ni Prof. Rudovick Kazwala kutoka SUA
0 Comments