SUAMEDIA

Prof. Kabudi afurahishwa kusikia kuwa SUA ndio yenye Hospitali pekee ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama


 Na: Calvin Gwabara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amepongeza kazi inayofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika kuboresha Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuleta tija kwa Taifa.



Mhe. Prof. Kabudi amesema hayo alipotembelea Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki AUGUST 1, 2020 kabla ya kwenda jukwaani kuzungumza na wananchi, waoneshaji na wadau wengine wa Kilimo wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo.

“Chuo Kikuu cha SUA mnafanya kazi nyingi na nzuri kwa faida ya nchi hii lakini niwaombe muongeze jitihada za kutangaza kazi hizi ili watu wengi wazijue na kunufaika nazo maana zinahitajika sana na wakulima, wafugaji na wavuvi”, alisisitiza Mhe. Prof. Kabudi.

Amesema kuna kila sababu ya SUA kuona umuhimu wa kuanzisha Mashamba ya Miti Dawa badala ya kutegemea kuvuna porini hivyo ziwepo jitihada za makusudi za kuhamasisha watu kupanda akitolea mfano nchi kama Madagaska ambao wameanza kutoa Miti Dawa porini  badala yake wamepanda Mashamba makubwa na sasa wanauza na kuipatia nchi hiyo dola milioni 14 kwa Mwaka.

Amesema anashukuru kwenye Ilani hii mpya ya Chama cha Mapinduzi kimeingiza mpango huo wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha miti Dawa hivyo ni muhimu kuanza kufikiria huko ili kujihakikishia Miti Dawa ya kutosha kiwanda hicho kitakapoanzishwa.

Mhe. Prof. Kabudi  amefurahi kusikia kwa mara ya kwanza kuwa SUA ndio yenye Hospitali pekee ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama na kwamba hili ni jambo kubwa ambalo Watanzania wanapaswa kulijua na kuitumia kikamilifu.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amemuonesha Mgeni rasmi Prof. Kabudi matrekta kumi ambayo SUA imepewa na Mhe. Rais Dkt.  John Pombe Magufuli na kusema kuwa yamekuwa chachu ya kuongeza mengine na vifaa mbalimbali vya kulimia na kufundishia kutokana na mapato ya ndani ya chuo hicho.

Post a Comment

0 Comments