Na: Farida Mkongwe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.
Palamagamba Kabudi ameitaka mikoa iliyopo Kanda ya Mashariki kuhakikisha
inatimiza majukumu yao katika uzalishaji wa mazao ili taifa liweze kusonga
mbele kiuchumi.
Akizungumza leo wakati akifungua Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Mashariki mkoani Morogoro Mh. Kabudi amesema mikoa hiyo ambayo ni Morogoro,
Tanga, Dar es Salaam na Pwani ina jukumu kubwa la kuzalisha mazao kwa wingi
yatakayowezesha viwanda kupata malighafi za kutosha katika kukuza viwanda
nchini.
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuinua uchumi
wa taifa hili, nchi yetu imeingia uchumi wa kati ni jukumu letu na hasa Kanda
ya Mashariki kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji huo”, amesisitiza
Mh. Kabudi.
“Kanda ya Mashariki inalo jukumu kubwa na muhimu la kupaisha
nchi, ni lazima muhakikishe mnachukua nafasi yenu, viongozi hakuna sababu ya
kuchekeana, tujifunge vibwebwe tufanye kazi kwa bidii ili maombi yetu ya kutaka
maonesho haya yaweze kufanyika kitaifa mwakani yaendane na jitihada zenu”,
amesema mh. Kabudi.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ametoa rai kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro kuepuka uharibifu
wa mazingira kwa kuacha tabia ya kujenga juu ya milima na kulima vyanzo vya
maji ili mkoa huo uweze kuwa na maji ya kutosha katika kuendeleza kilimo.
Aidha Mh. Kabudi pia amewataka wakulima, wafugaji na wavuvi
wanaoshiriki katika maonesho hayo kuanza kulima miti dawa au mimea dawa ambayo
kwa kiasi kikubwa ambayo imetumika kudhibiti janga la ugonjwa wa corona hapa
nchini na kusema kuwa miti hiyo itakuwa na soko kubwa baada ya miaka mitano
kutokana na umuhimu wake katika tiba.
Maonesho ya wakulia, wafugaji na wavuvi kwa mwaka huu 2020
yamebeba kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua
Viongozi Bora 2020”.
0 Comments