Na: Farida Mkongwe
Jaji Mkuu Mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mh. Mohamed Othman Chande amempongeza aliyekuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) Prof. Peter Gillah kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake katika kipindi chake cha uongozi.
Mh. Chande ametoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kumpongeza na kumtakia heri Prof. Gillah ambaye amestaafu wadhifa huo tarehe 30 mwezi 4 mwaka huu baada ya kutumikia nafasi hiyo kuanzia tarehe 1 Julai, 2011 ikiwa ni zaidi ya miaka 8
“Kuna sera nyingi za chuo ambazo Prof. Gillah ameshiriki katika uanzishwaji wake, kiukweli mchango wake ni mkubwa na natambulika hapa chuoni, nimpongeze tu kwa ubunifu wake, uvumilivu wake na usikivu wake ambao leo hii umetufikisha hapa tulipo”, alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mh. Chande.
Awali akitoa salaam kwa wanajumuiya wa chuo na kumkaribisha mgeni rasmi, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Pro. Raphael Chibunda amesema Prof. Gillah atakumbukwa kwa uchapakazi wake kwani alikuwa ni mtu jasiri, hodari na mwenye kusimamia majukumu yake.
“Prof. Gillah ni mtu ambaye akisimamia jambo basi ni kweli jambo hilo litatekelezeka, Profesa niwe mkweli nitakumiss sana kwani wewe ni mtu wa aina yake”, alisema Prof. Chibunda.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Prof. Gillah, Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Dkt. Suzana Augustino amesema Prof. Gillah amefanikiwa kuandaa na kutekeleza Mpango Mkakati wa Chuo wa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2016/17 hadi 2020/21, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kutoka 5,563 mwaka wa masomo 2011/2012 hadi kufikia wanafunzi 13,166 kwa mwaka wa masomo 2019/2020.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa shahada za mafunzo yanayotolewa chuoni katika ngazi mbalimbali, kukiwezesha chuo kupata miradi mikubwa ya utafiti, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali pamoja na kukua na kupanuka kwa ushirikiano kati ya chuo na taasisi mbalimbali ndani na nje ya chuo.
Kwa upande wake Prof. Gillah amekishukuru chuo cha SUA kwa kutambua mchango wake huku akitoa wito kwa viongozi na wafanyakazi wa chuo hicho kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili waweze kutekeleza ipasavyo majukumu yao na hatimaye waweze kufikia malengo ya chuo.
Sherehe hiyo ya kumpongeza na kumtakia heri Prof. Gillah ilienda sanjari na kumuaga aliyekuwa Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha Prof. Yasinta Muzanila, kumkaribisha rasmi Prof.
Amandus Muhairwa ambaye kwa sasa ndiye Naibu Makamu Mkuu wa chuo Utawala na Fedha pamoja na kumkaribisha Prof. Maulid Mwatawala ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa
Taaluma.
0 Comments