Na Gerald Lwomile
Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Mhe. Antony Mtaka amesema utafiti unaofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo SUA kuhusu kutumia bundi kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao kama panya
na wengine si tu utawasaidia wakulima kuongeza mavuno lakini pia utaondoa imani
potofu juu ya mnyama huyu
Bundi akiwa ndani ya boksi lililotengezwa maalum
Akizungumza wakati akitembelea banda la Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo SUA katika viwanja vya Maonesho, Nyakabindi, Bariadi mkoani
Simiyu Mtaka amesema kwa muda mrefu kumekuwa na imani kuwa ndege huyo anapotua katika
eneo fulani basi eneo hilo hutokea kifo
Amesema matokeo ya utafiti huu utainufaisha jamii ya
kitanzania ukizingatia kuwa SUA
inaendelea na juhudi za kueneza ubunifu huu wa kuwatumia bundi kudhibiti wadudu hai waharibifu wa mazao hususani panya na wadudu wengineo na hapana shaka ndege
huyo ataonekana ni rafiki wa binadamu badala ya kuwa adui
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka wa tatu mbele kulia akisikiliza maelezo kutoka kwa Prof. Loth Mulungu wa kwanza kulia
Akizungumzia utafiti huo, Prof. Loth Mulungu amesema kwa
kawaida bundi huwa na uwezo mkubwa wa kuona wakati wa usiku na hukaa eneo la
juu ili kupanua wigo wa kuona wa kutafuta chakula chake, ambapo panya ni miongoni vya chakula chake
“Bundi mmoja anauwezo wa kula panya mmoja mpaka kumi na mbili kwa siku na kutokana na uwezo wake wa kusafiri hadi kilomita nne (4) nasi tumekadiria kuwa anaweza kutembelea hekta 350 za mashamba sasa hiyo ndiyo faida kubwa ya bundi katika kumsaidia mkulima lakini pia anapotoa sauti yake panya hawawezi kutoka katika mashimo na kula mazao ya mkulima ” amesema Prof. Mulungu
Prof. Mulungu amesema mbali na kula panya, bundi hula
wadudu wengine kama vile panzi na nzige
Akizungumzia namna ya kumvutia bundi kukaa na anabaki
katika eneo la mkulima amesema ni kutengeneza masanduku yenye uwazi kama mlango
hivi kwa hiyo bundi atakuwa akiingia na kutaga katika eneo hilo
“Mkulima pia anaweza kuweka kitu kama kigogo hivi kirefu katika shamba ili bundi anaposafiri kutoka kwenye kiota chake aweze kutua katika kigogo hicho na kujitafutia chakula chake” amesema Prof. Mulungu
Prof. Mulungu amewatoa hofu wakulima na wananchi na
kuwambia bundi ni ndege rafiki na hivyo imani za kuwa ndege huyo anatumika kwa
mambo ya usharikina zimepitwa na wakati
0 Comments