Na: Tatyana Celestine.
Wakazi wa Kijiji cha Wami Dakawa Halmashauri ya
Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wameushukuru Ushirika wa Vijana Wahitimu wa
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUGECO, kwa kuwapatia madawati na vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya
shilingi Million nane na laki tano (8,500,000/=) katika Shule Shikizi ya Msingi Mtakuja Bwawani
iliyojengwa na wahisani kwa ushirikiano na wananchi.
Akikabidhi madawati hayo Mkurugenzi wa
SUGECO Revocatus Kimario amesema SUGECO imeguswa kutoa msaada huo baada ya kuona
vijana wengi watokao kijijini hapo hawajui kusoma na kuandika sambamba na
mazingira ya shule hiyo yasiyoridhisha ambapo wanafunzi wanalazimika kukaa
chini kwa kukosa madawati.
“SUGECO tunaamini ni muda muafaka sasa shule hii
shikizi kupandishwa hadhi na kusajiliwa rasmi ili iweze kuwasaidia wananchi wa
eneo hili, na wito wetu kwa halmashauri ikiwapendeza kuona namna ya kuifanya
shule rasmi na wadau wote wakiwemo wazazi na wananchi kuendelea kujitolea kwa
hali na mali kukamilisha uwekaji wa miundombinu muhimu ili kufanikisha azma ya
kuwa na shule katika eneo lao”. Alisema Kimario.
Wanafunzi wa shule shikizi ya kihonda bwawani wakifurahia madawati yaliyoletwa shuleni hapo na SUGECO baada ya kukabidhiwa shuleni hapo |
Nae Mkazi wa kitongoji hicho Bwana Rajab Simba anayeishi
eneo la Bwawa la Kihonda Kitongoji cha Kibao cha Ranchi amedai kuwa pamoja na
uwepo wa kaya zaidi ya elfu tatu hakuna huduma muhimu za kijamii kama shule,
zahanati na kwamba wanalazimika kufuata huduma kwa umbali wa zaidi ya kilomita
20.
“Kutokana na umbali kutoka hapa Bwawa la Kihonda
mpaka Wami Sokoine ilipo shule ya msingi zaidi ya kilomita 25 wazazi tuliamua
kuanzisha shule ambayo ni mkondo wa shule ya msingi Wami Sokoine ambapo walimu
wanaofundisha ni wakujitolea kwa kulipwa na wanakijiji”, alisema Rajab Simba
Mpaka sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 225
kuanzia awali mpaka darasa la saba, ikiwa na vyumba vitatu vya madarasa ambapo
ni darasa moja pekee lililo ezekwa.
Nae Mwalimu Mkuu wa shule hiyo shikizi Betrice
Masawe amesema kwa sasa kuna walimu saba wakujitolea na
changamoto iliyopo ni umbali kutoka eneo hilo hadi ilipo shule mama ya Wami Sokoine
ambako wanafunzi wa darasa la nne na saba hulazimika kuhamia huko kipindi cha
mitihani ya kitaifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero
Albinus Mgonya ambaye amepokea madawati hayo kwa niaba ya wananchi hao mbali na
kukiri umbali uliopo kutoka eneo hilo la Bwawa la Kihonda hadi Kijiji cha
Dakawa zilipo huduma za kijamii, amesema miongozo ya kusajili eneo lolote la
Utawala ipo wazi akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutumia wataalam
katika sekta hiyo kutoa miongozo katika utekelezaji.
“Kama ilivyo miongozo ya kusajili maeneo ya
utawala, hata kwenye taratibu za kusajili shule miongozo ipo wazi nikutake Mkurugenzi
uwalete wataalam wako hapa ili wawaongoze wananchi kuainisha sifa
zinazohitajika ili kuona kama kuna uwezekano wa kusajili shule hii”,alisema
mkuu huyo wa Wilaya ya Mvomero.
0 Comments