SUAMEDIA

Matumizi ya Akili Bandia kufanya Kilimo cha Usahihi kupunguza gharama za Uzalishaji

              

Na, Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Idara ya Uhandisi Kilimo imekuja na Roboti linalojiendesha lenyewe lenye uwezo wa kupiga dawa ya kuuwa magugu au wadudu kwenye sehemu husika pekee kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika Viwanja wa Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.



Hayo yamebainishwa na  Donat Shukuru Mkufunzi Msaidizi toka Shule ya Uhandisi na Teknolojia, Idara ya Uhandisi Kilimo SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho hayo kuhusiana Vumbuzi mbalimbali wanazozifanya ikiwemo Mashine za Teknolojia za kisasa au Mashine zinazotumia Akili bandia pamoja na Mifumo mbalimbali itakayoleta Tija kwenye Kilimo.

Amesema lengo la kuleta Teknolojia hiyo ya Roboti ni kuhakikisha Kilimo kinafanyika kwa usahihi kwa kuwa inaenda kuokoa gharama za Uzalishaji kwa kupunguza matumizi ya dawa vile vile kusaidia kuondoa matumizi ya dawa yasiyohitajika kwenye Mazingira kwa kuwa kuweka dawa kwenye Mazingira bila kujua ni kiasi gani kinachohitajika ni kuchafua Mazingira.

Vile vile kwa kuwa Roboti hilo linajiendesha lenyewe linakuwa linamuweka mbali  mtumiaji wa dawa na kumuepusha kuathirika na dawa hizo hivyo inaonesha ni jinsi gani Teknolojia hiyo ilivyo ya muhimu na kuleta Tija kwenye Kilimo. 

“Tunahusika pia na Vumbuzi mbalimbali kama Mashine za kutotoreshea Vifaranga, Mashine za kuangulia mayai kama ni mazima, Mashine za automatic za Umwagiliaji (Automatic irrigation system) vile vile tunahusika na Mifumo mbalimbali ya simu kama vile Mifumo ya kushauri kiasi cha maji cha Umwagiliaji na Mifumo ya kuangalia Magonjwa kwenye Mimea”, amesema Mkufunzi huyo. 



Post a Comment

0 Comments