SUAMEDIA

Wakulima watakiwa kutumia Darasa Mtandaoni ili kuepuka gharama

Na: Farida mkongwe

Wakulima nchini wamehamasishwa kujiunga na mfumo wa Darasa Mtandaoni ambao unamuwezesha mkulima kupata mafunzo kwa njia ya mtandao bila kutoka sehemu moja kwenda nyingine na hivyo kupunguza gharama zinazoweza kuepukika.

Hamasa hiyo imetolewa Agosti 6, 2023 na Mkufunzi Msaidizi kutoka Shule Kuu ya Elimu Idara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia SUA Juma Halfan Fundikira wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu faida za mfumo huo katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mjini Morogoro. 

Bw. Fundikira amesema katika mfumo huo kunakuwa na wataalamu wanaojiunga hivyo mkulima naye anapokuwa kwenye darasa mtandao anaweza kupata elimu kwa gharama ndogo bila kulazimika kusafiri.

“Karibuni sana banda la SUA katika Idara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hapa tunatoa elimu ya Darasa Mtandaoni ambapo mkulima hata akiwa kijijini au sehemu nyingine yoyote anaweza kupata elimu bila kufunga safari na kuja eneo husika”, amesema bw. Fundikira.

Amesema wanajaribu kuwashawishi wakulima na watanzania kwa ujumla  waweze kuwa na mwamko wa kutumia fursa kama hizo kwa sababu Dunia inabadilika, Sayansi na Teknolojia inakua na kwamba hakuna maendeleo bila ya kuwa na Sayansi na Teknolojia ndio maaana wanajaribu kushirikiana na wadau tofauti ili kuweza kumfikia mkulima na kumfikishia elimu.

Akizungumzia changamoto zilizopo kwenye matumizi ya mfumo huo Bw. Fundikira amesema mwitikio wa watu bado sio mkubwa sana na hasa maeneo ya vijijini ambako wanamiliki simu lakini unakuta ile simu haitumii mtandao. 

“Watu wengine unakuta kweli simu zao hazitumii mtandao lakini wengine wanapuuzia tu kwamba anaona atatumia gharama au anaona atatozwa pesa lakini hawajui pengine mafunzo haya yanatolewa bure au kwa gharama ndogo sana tofauti na angefunga safari angeenda kwenye chuo, anasahau kwamba faida ya Darasa Mtandaoni ni kwamba mkulima angeweza kusoma au kujifunza bila kuacha shughuli zake”, amesema Bw. Fundikira.








Post a Comment

0 Comments