Na: Farida mkongwe
Imeelezwa kuwa Elimu ya Kilimo
cha Umwagiliaji katika maeneo yenye Miinuko inayotolewa na Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) iwapo itazingatiwa ipasavyo itakuwa ni njia tosha ya
kumuwezesha mkulima wa maeneo hayo kulima na kupata mazao yenye tija pamoja na
kutunza mazingira.
Hayo yameelezwa Agosti 6, 2023 na Mhadhiri kutoka Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Khalifan Hassan Hamidu wakati akizungumza na SUAMEDIA katika banda la SUA kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mjini Morogoro.
Dkt. Hamidu amesema katika
banda hilo wanaonesha namna wanavyowaandaa Maafisa Ugani wanaojifunza kuwa
walimu katika sehemu mbalimbali ikiwemo sehemu ambazo zina wakulima kuendesha
kilimo cha umwagiliaji bila wakulima kulalamikia uhaba wa maji au mazao kutokuwa
vizuri kwa sababu hakutakuwa tena na
changamoto ya ukosefu wa maji.
“Kwa mfano Afisa Ugani anataka
kwenda kufundisha au kuelekeza kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo ya miinuko
au pembezoni mwa milima, jambo la kwanza atachimba bwawa litakaloweza kutunza
maji kwa mwaka mzima ambapo chanzo chake kitakuwa ni mvua au chemichemi, pia
atatengeneza mfereji ambao kwa mbele utaunganishwa na vijaruba vitatu, cha kwanza
kitakuwa karibu na bwawa, cha pili kitakuwa mbali kidogo na bwawa na cha tatu
kitakuwa bondeni kidogo mwa mteremko wa mlima”, amesema Dkt. Hamidu
Amesema baada ya hatua hiyo
Afisa Ugani atatengeneza mageti, geti la
kwanza litakuwa na kizuizi cha maji yasiendelee kwenda bondeni kwenye mfereji
mkuu lakini kunakuwa na mfereji mdogo unaoingia kwenye kijaruba cha kwanza kwa
hiyo ataweka hicho kizuizi cha maji kinachozuia maji yasiende bondeni ila
atafungua kile kizuizi cha maji ambacho kinapeleka maji kwenye kijaruba cha
kwanza ambacho amepanda aina ya kwanza ya zao kwa sababu anaweza kuwa na
vijaruba kama vitatu au vinne akapanda mazao tofauti.
“Kwa hiyo atafungua maji katika
kiwango atakachoona yeye kinafaa ili kutunza maji na kuzuia maji yasipotee
akimaliza atafunga, atafungua tena kwenye kijaruba kingine mpaka anamaliza, hii
inasaidia sana kutunza maji yasipotee pande zote za shamba upande wa bondeni na
upande wa mwinuko na kilimo hiki anaweza kukifanya kwa muda wa miaka mitatu”, amesema
Mhadhiri huyo.
Amesema Afisa Ugani anayewaelimisha watu anapaswa awaelimishe kwa
vitendo akiwa na zana au kifaa ambacho kinasaidia kuwafanya wakulima au
wanafunzi waelewe kwa kuona , kwa kujaribu na kutenda na ndio maana na wao
wamekuja na zana hizo katika Maonesho hayo ya Nanenane.
0 Comments