SUAMEDIA

Waziri Mkuu kufunga maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH Novemba 18, 2026

Na: Farida Mkongwe

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kitakachofanyika Novemba 18 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema shughuli za kilele zitafanyika Novemba 17 na 18, zikijumuisha maonesho ya tafiti, teknolojia na bunifu zinazolenga kutatua changamoto za wananchi.

Prof. Mkenda amesema maadhimisho hayo yametoa nafasi ya kutathmini mchango wa COSTECH katika maendeleo ya nchi na kuweka msukumo mpya wa matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuwa shughuli zilizofanyika kuelekea kilele hicho ni pamoja na kliniki ya ubunifu wakati wa maonesho ya Nanenane, maonesho katika viunga vya Bunge na mikutano ya wadau wa sayansi na utafiti.

Miongoni mwa bunifu alizozitaja ni mkanda wa kusaidia kudhibiti upotevu wa damu kwa mama baada ya kujifungua na chanjo ya samaki inayolenga kukabiliana na magonjwa yanayoathiri ufugaji wa samaki.

Pia ametaja ubunifu wa kuzalisha gesi kwa kutenganisha hidrojeni na oksijeni kutoka kwenye maji, akieleza kuwa ameagiza wataalamu kuchunguza usalama wake pamoja na uwezekano wa matumizi yake kiuchumi na kibiashara.

Katika eneo la afya, Prof. Mkenda amesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kufanya uchunguzi wa kisayansi kuhusu mimea inayotumika kutibu magonjwa, ili kubaini ufanisi, kiwango sahihi cha matumizi na madhara yanayoweza kujitokeza.

Amesema ni muhimu kuimarisha uwezo wa kufanya majaribio ya awali ya dawa nchini kabla ya kufikia hatua ya kuzijaribu kwa binadamu, ili kuongeza mchango wa watafiti wa Tanzania katika maendeleo ya tiba.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia yanapaswa kuimarishwa pia katika kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji wa madini, ili kuongeza tija na kujenga uwezo wa nchi kutumia rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi.

Ameeleza kuwa katika kilimo, utafiti na teknolojia vinapaswa kusaidia kuongeza uzalishaji katika eneo linalolimwa, kupunguza umaskini wa wakulima na kuchangia upatikanaji wa chakula kwa gharama nafuu.

Aidha, ametaja ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship, utoaji wa tuzo kwa watafiti na Mfuko wa Samia wa Ubunifu kuwa miongoni mwa jitihada za kuendeleza wataalamu na kuwawezesha wabunifu nchini.

Prof. Mkenda amewakaribisha wananchi, waandishi wa habari na wadau mbalimbali kutembelea maonesho hayo Mlimani City Novemba 17 na 18, ili kujionea mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya Tanzania.


Post a Comment

0 Comments