SUAMEDIA

Watafiti Afrika waunganisha nguvu kuimarisha tafiti za kilimo ikolojia

Na: Farida Banzi

Watafiti na wadau wa kilimo kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameungana kupitia mitandao ya ushirikiano wa kisayansi ili kuimarisha tafiti za kilimo ikolojia, kubadilishana teknolojia na maarifa, pamoja na kutafuta suluhisho za changamoto zinazowakabili wakulima.

Ushirikiano huo unalenga kukuza uzalishaji endelevu, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pamoja na kuboresha maisha ya wakulima barani Afrika.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala, amesema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kuendeleza tafiti na ubunifu unaolenga kuleta mageuzi endelevu katika kilimo.

Prof. Mwatawala amesema SUA inajivunia kuwa kitovu cha uratibu wa shughuli za kilimo ikolojia nchini Tanzania, hali inayoweka msingi wa kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi katika kuendeleza tafiti zenye manufaa kwa wakulima na jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhawilishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu wa SUA, Prof. Japhet Kashaigili, amesema taasisi za utafiti zinahitaji kuunganisha nguvu, uzoefu na rasilimali ili kuongeza tija katika tafiti za kilimo ikolojia.

Ameeleza kuwa kufanya kazi kwa kujitenga kunapunguza fursa za kupata matokeo yanayotarajiwa, hivyo ushirikiano unahitajika katika kubaini changamoto na kuandaa suluhisho zinazokidhi mahitaji ya jamii.

Prof. Kashaigili ameongeza kuwa SUA inaendelea kushirikiana na wadau kupitia mitandao ya kikanda inayounganisha watafiti wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ili kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa na kuibua miradi ya pamoja.

Naye Mwanasayansi Mwandamizi kutoka Kituo cha Kimataifa cha Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (icipe), ambaye pia ni Mtafiti Mkuu wa Mtandao wa Kikanda wa Utafiti wa Kilimo Ikolojia Afrika Mashariki, Dkt. Frank Chidawanyika, amesema majukwaa ya kisayansi yanatoa fursa kwa watafiti, wanafunzi na taasisi kushirikiana katika kuandaa miradi, kupata rasilimali na kujenga uwezo wa kitaalamu.

Ametaja mfano wa mafanikio ya ushirikiano huo katika mtandao wa utafiti wa Afrika Kusini, ambao amesema umewezesha kuandaliwa kwa zaidi ya miradi 30 ya pamoja, usimamizi wa pamoja wa zaidi ya wanafunzi 50 wa shahada za uzamili na uzamivu, pamoja na kuchapishwa kwa zaidi ya makala 150 za kisayansi zilizopitiwa na wataalamu.

Kwa upande wake, Meneja wa Programu za Kisayansi wa Shirika la Utafiti wa Kilimo kwa Maendeleo la Ufaransa (CIRAD), ambaye pia ni Mratibu wa Jukwaa la Kikanda la TRACE kuhusu Kilimo Ikolojia na Afya Afrika Mashariki, Dkt. Eglantine Fauvelle, amesema majukwaa hayo yanalenga kuunganisha uwezo wa taasisi, wanasayansi na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali ili kuimarisha tafiti na ubunifu.

Ameeleza kuwa TRACE ni miongoni mwa majukwaa mapya yanayolenga kuwakutanisha wadau wa kilimo ikolojia na maendeleo, kujenga ushirikiano wa wataalamu wa taaluma mbalimbali na kuandaa mapendekezo ya miradi ya pamoja.

Dkt. Fauvelle ameongeza kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa taasisi za utafiti, kupunguza kurudiwa kwa tafiti zinazofanana na kuboresha matumizi ya rasilimali zilizopo.

Kupitia mitandao hiyo, watafiti wanatarajia kuzalisha maarifa na teknolojia zinazozingatia mazingira na mahitaji halisi ya wakulima. Jitihada hizo zinalenga kuongeza uzalishaji na tija, kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mchango wa kilimo katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii barani Afrika.






Post a Comment

0 Comments