SUAMEDIA

Wanafunzi wapya SUA wafurahishwa na mapokezi kituo cha mabasi Msamvu

 Na: Ngolo Mboje

Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo 2026/2027 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza kufurahishwa na mapokezi waliyopatiwa na chuo hicho katika kituo cha mabasi cha Msamvu, mkoani Morogoro, wakisema huduma hiyo imewasaidia kufika chuoni kwa usalama na kuepuka hatari ya kutapeliwa.

Wakizungumza wakati wa mapokezi hayo, Adili Stanuel na Grace Grayson, wanaotarajia kujiunga na Shahada ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji (Bachelor of Science in Animal Science and Production), wamesema utaratibu huo umewapa faraja na kuondoa hofu ya kukumbana na watu wasio waaminifu wanapowasili katika mazingira mapya.

Wanafunzi hao wamesema wana matumaini ya kufanya vizuri katika masomo yao, kujenga ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzao katika shughuli za kitaaluma na kijamii, pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za chuo.

“Tunatumaini kupata maarifa na uzoefu utakaotuwezesha kuchangia katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kibiashara baada ya kuhitimu masomo yetu, pia, tunatarajia kuwa na ushirikiano mzuri katika masuala mbalimbali ya kitaaluma na kijamii,” wamesema.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea na utaratibu wake wa kila mwaka wa kuwapokea wanafunzi wapya katika vituo vya mabasi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanafunzi hao wanapata mwongozo sahihi na kufika chuoni kwa usalama wanapowasili mkoani Morogoro.

Utaratibu huo unalenga pia kuwasaidia wanafunzi wapya kuzoea mazingira ya chuo, kupunguza changamoto wanazoweza kukumbana nazo wanapowasili kwa mara ya kwanza, pamoja na kuwalinda dhidi ya vitendo vya utapeli vinavyoweza kufanywa na watu wasio waaminifu.




Post a Comment

0 Comments