Na: Farida Mkongwe
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cardiff nchini Uingereza wamependekeza kuimarishwa kwa usimamizi wa maji chini ya ardhi na kuangaliwa kwa uwezekano wa kuunganisha visima binafsi na mfumo rasmi wa usambazaji wa maji, ikiwa ni hatua ya kuongeza ustahimilivu wa Jiji la Dodoma dhidi ya changamoto ya upungufu wa maji.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti wa Ustahimilivu wa Maji katika Miji katika warsha ya kuwasilisha matokeo kwa wadau iliyofanyika Oktoba 15, 2026, jijini Dodoma, Kiongozi wa Mradi kutoka Chuo Kikuu cha Cardiff nchini Uingereza Dkt. Adrian Healy amesema utafiti huo umeonesha kuwa visima binafsi vina mchango muhimu katika kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi na shughuli za kiuchumi, hususan katika maeneo ambayo huduma za maji ya mabomba hazijafika au hazitoshelezi mahitaji yaliyopo.
Dkt. Healy amesema kutokana na matokeo hayo, watafiti wanapendekeza kuangaliwa kwa mfumo mchanganyiko wa usambazaji wa maji unaojumuisha mtandao rasmi wa mabomba na visima binafsi vinavyotumia maji chini ya ardhi, badala ya kutegemea kuongeza pekee kiwango cha maji yanayosafirishwa kutoka vyanzo vilivyo mbali. Amesema mfumo huo unaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja na kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinaendelea hata wakati wa upungufu wa maji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti zaidi kuhusu kiwango cha maji kinachopatikana chini ya ardhi, ubora wake na uwezo wa vyanzo hivyo kujazwa upya, ili kuwezesha matumizi endelevu bila kuathiri akiba ya maji. Ameeleza kuwa kuongezeka kwa visima binafsi bila usimamizi wa kutosha kunaweza kusababisha uchotaji mkubwa wa maji, kuathiri visima vya maeneo jirani na kuongeza hatari ya kupungua kwa rasilimali hiyo katika siku zijazo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Healy amependekeza kuchunguzwa kwa fursa za kutumia maji yaliyotibiwa baada ya matumizi katika hoteli, ofisi, majengo makubwa na maeneo ya biashara kwa shughuli zisizohitaji maji ya kunywa, kama vile kusafisha vyoo, kumwagilia bustani na kuosha magari. Amesema hatua hiyo inaweza kupunguza matumizi ya maji safi katika shughuli ambazo zinaweza kutumia maji ya ubora tofauti, hivyo kupunguza shinikizo kwa vyanzo vikuu vya maji.
Ameongeza kuwa uzoefu wa miji ya Cape Town nchini Afrika Kusini na Windhoek nchini Namibia unaonesha umuhimu wa kuwa na vyanzo mbalimbali vya maji pamoja na mifumo ya kuhifadhi maji chini ya ardhi kwa ajili ya matumizi wakati wa ukame na dharura. Amesema Dodoma inaweza kujifunza kutokana na mifumo hiyo na kuchunguza namna teknolojia za kurejeleza na kuhifadhi maji zinavyoweza kuimarisha usalama wa maji kwa muda mrefu.
Dkt. Healy amesema utafiti huo pia umeibua umuhimu wa kuzingatia usawa katika upatikanaji wa maji, kwa kuwa si kaya zote zenye uwezo wa kifedha wa kuchimba visima binafsi. Ameeleza kuwa ingawa baadhi ya wamiliki wa visima huwapatia majirani maji, upatikanaji wa huduma hiyo unategemea makubaliano ya wahusika, hivyo kuna haja ya kuwa na mifumo bora ya usimamizi itakayolinda maslahi ya watumiaji wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji, Mhandisi Robert Sunday, amesisitiza umuhimu wa kutumia matokeo ya tafiti katika kuandaa sera na mikakati ya usimamizi wa rasilimali za maji, huku akiwahimiza watafiti kuendeleza tafiti kuhusu maji chini ya ardhi kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo sayansi ya isotopu inayosaidia kubaini asili, ubora na namna maji yanavyojazwa upya ardhini.
Amesema usalama wa maji ni msingi wa maendeleo endelevu ya miji na ukuaji wa uchumi, hivyo ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu na taasisi za utafiti unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika katika kutatua changamoto halisi za wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Utafiti huo umeibua mjadala kuhusu nafasi ya visima vya kaya, visima vya jamii na visima vinavyotumiwa na taasisi na wafanyabiashara katika mfumo wa baadaye wa usambazaji wa maji jijini Dodoma, huku ukisisitiza umuhimu wa kuzingatia uendelevu wa vyanzo, usalama wa maji na usawa katika upatikanaji wa huduma.
Picha na Ttayana Celestine. Zaidi bofya link hapa chini
0 Comments