Na: Ngolo Mboje
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa
kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu nchini kupitia mradi wa HEET,
kimetoa mafunzo kwa vijana kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na mifumo ya
kidijitali. Mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia kutambua fursa za kiuchumi na
kutumia teknolojia kujiajiri.
Dkt. Jaffari amesema mafunzo hayo yanachangia
kukuza ujuzi, fikra bunifu na uwezo wa vijana kutumia teknolojia kutatua
changamoto katika jamii. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira
ya kujifunzia ili vijana wapate ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa.
Amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii na mifumo ya kidijitali zaidi ya kufanya mawasiliano, kwa kubuni bidhaa na huduma, kuzalisha maudhui, kufanya utafiti na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowazunguka.
Kwa upande wake, Profesa Samweli Kabote, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, amesema mafunzo hayo yatawaongezea vijana uwezo wa kutumia teknolojia kutengeneza fursa za kiuchumi.
Amesema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wasomi
nchini, ni muhimu vijana kutumia maarifa na ujuzi walionao kujiajiri badala ya
kutegemea ajira rasmi pekee.
Naye Mratibu wa Taifa wa Teknolojia za Kidijitali katika Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Alcardo Barakabitze, amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa vijana kutumia teknolojia katika kujifunza, kufanya kazi na kuendesha shughuli za ujasiriamali.
Mmoja wa washiriki, Ally Abdallah, amesema mafunzo
hayo yamemfungua macho kuhusu fursa ambazo awali hakuzifahamu. Ameeleza kuwa
amejifunza namna ya kutumia simu ya mkononi na kompyuta kufanya shughuli za
kidijitali zinazoweza kumwezesha kujiajiri.
0 Comments